Jela maisha kunajisi mtoto wa miaka minne

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:09 AM May 07 2024
Jela maisha kwa kunajisi mtoto.
PICHA: MAKTABA
Jela maisha kwa kunajisi mtoto.

FADHILI Shaibu (36), mkazi wa kijiji cha Chiwale wilayani Masasi, mkoani Mtwara amehukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kukutwa na hatia ya kumnajisi mtoto wa kike wa kaka yake mwenye umri wa miaka minne, baada ya kumrubuni kuwa atampa machungwa.

 Hukumu hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki mjini Masasi na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Masasi, Batista Kashusha, baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote na kujiridhisha na vielelezo vya ushahidi vilivyotolewa mahakamani na upande wa Jamhuri pamoja na upande wa mashtaka.

Akisoma hukumu hiyo, Kashusha alisema kuwa kesi hiyo namba 93 ya mwaka 2023 ilikuwa na mashahidi watano, na kwamba mahakama imemtia hatiani mshtakiwa kwa kumhukumu kifungo cha maisha jela baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo.

Ilidaiwa mahakamani humo kuwa mshtakiwa alifanya kosa la kumnajisi mtoto wa kaka yake Agosti 25, mwaka 2023 majira ya saa 9:30 jioni wakati akiwa nyumbani kwake katika Kijiji cha Chiwale, Halmashauri ya Wilaya ya Masasi na kumsababishia maumivu makali na kumharibu sehemu za siri.

Kabla ya hukumu hiyo, Hakimu alisoma maelezo ya awali akieleza kuwa siku ya tukio alifika nyumbani kwa mtoto na kumkuta mama wa mtoto ambaye ni shemeji yake akiwa na mtoto huyo ndipo alipomchukua na kuondoka naye akidai kuwa anakwenda kumnunulia machungwa kwa madai kwamba mara kwa mara alikuwa akimwomba amnunulie machungwa.

Hakimu Batista alisema mshtakiwa alipofika nyumbani kwake majira ya saa 9:30 alasiri aliingia naye chumbani kwake na kuanza kumnajisi mtoto huyo na mtoto akiporudi nyumbani alimwelezea mama yake kitendo alichofanyiwa na mshtakiwa ambaye ni baba yake mdogo.

Alisema hukumu hiyo imezingatia vipengele vyote vya msingi vya kisheria ikiwa ni pamoja na ushahidi wa kitabibu uliotolewa na daktari aliyemfanyia vipimo vyote mtoto aliyefanyiwa tukio hilo pia ushahidi mwingine ulitolewa na mama mzazi wa mtoto na mtoto mwenyewe na kwamba kwa ushahidi huo mahakama imetoa kifungo hicho kwa mshtakiwa pasipo na shaka yoyote.

Katika maelezo ya awali, Mkuu wa Mashtaka Wilaya ya Masasi ambaye ni wakili wa serikali mwandamizi Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) Wilaya ya Masasi, Miraji Kajieuli, aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwa wengine wanaofanya vitendo kama hivyo vya kinyama.

Wakili Kajieuli alisema mshtakiwa alipaswa kuwa mlezi mwema kwa mtoto huyo na wengine waliopo katika jamii, lakini amegeuka na kuwa mnyama na kumnajisi mtoto jambo ambalo amemsababishia athari za kimwili na kisaikolojia.

Mshtakiwa huyo alivyopewa nafasi ya kujitetea, aliiomba mahakama kumwachia huru kwa kuwa hajatenda kosa hilo na kwamba kifungo cha maisha jela kitamwathiri kimaisha kwa kuwa ana mke na watoto watatu wanaomtegemea.

Mwisho