Kanisa la wasabato kutoa elimu ya afya ya akili kwa waumini wao

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 05:39 PM May 08 2024
Katibu Mkuu wa Kanisa la Adventista Wasabato Jimbo Kuu la Kaskazini mwa Tanzania Mchungaji Magulilo Mwakalonge akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake.
Picha: Maktaba
Katibu Mkuu wa Kanisa la Adventista Wasabato Jimbo Kuu la Kaskazini mwa Tanzania Mchungaji Magulilo Mwakalonge akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake.

KANISA la Adventista Wasabato (SDA Tanzania), lililopo kata ya Nyahanga Halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, limeanzisha maombi maalumu ya siku 21 ili kutoa elimu ya mambo mbalimbali ikiwemo afya ya akili pamoja na kujua njia ya upatikanaji wa matibabu yake.

Elimu hiyo itaanza kutolewa Mei 11 hadi juni mosi mwaka huu, na itakuwa ikirushwa katika vyombo mbalimbali vya habari kupitia lugha nne za kimataifa ikiwemo Kiarabu, Kingereza, Kifaransa na kiswahili huku kongomano hilo likipewa jina ‘Yatosha Jangwani’

Katibu Mkuu wa Kanisa la Adventista Wasabato Jimbo Kuu la Kaskazini mwa Tanzania, Mchungaji Magulilo Mwakalonge, ameyabainisha hayo leo wakati akizungumza na vyombo vya habari katika Ofisini ndogo ya kahama huku akiwakaribisha waumini na wananchi kujitokeza na kupata elimu ya afya ya akili, mahusiano na mawalezi ya watoto, mada za watoto na Neno la Mungu lenyewe.

Amesema, kila mmoja ni mhanga wa afya ya akili isipokuwa hawatambui kiwango cha afya ya akili mwilini, hivyo wameamua kutoa elimu hiyo ili kuwajenga waumini kiafya na kuwa tayari kupokea neno la Mungu na kulihifadhi na wale watakaojihisi wanashida wanapewa elimu ya namna ya kuepuka tatizo hili ili lisiendelee kuwa kubwa zaidi.

Aidha, Mwakalonge amesema, elimu ya namna hiyo wameshaitoa Juba, Nyamongo, Babati na sasa ni zamu ya Kahama, nakwamba matatizo mengi tunayoyapitia yanatokana na afya ya akili na inapokuwa na shida ni ngumu waumini kupokea neno la Mungu na kuwasihi kujitokeza siku hiyo.

"Tutakuwa na mtaalamu wa magonjwa ya afya ya akili ambae atatoa elimu hii kwa kipindi chote, waumini na wananchi watakaohudhuria watapata fursa ya kuuliza maswali ili wapate kujifunza zaidi na itakuwa ikitafasiriwa pia kwa lugha za kiarabu, kifaransa, kingereza na kiswahili chenyewe ili kuwapata fursa wananchi wa mataifa mengine kujitunza pia" amesema.

Mmoja wa waumini wa kanisa hilo, Valelia Mwaja amesema, atahudhuria vipindi vyote vitavyofundishwa hususani ya afya ya akili ili kujifunza na kutambua viashiria vyake na atakuwa na mwanga wa kuwaelimisha watu wengi wasiojua na kuacha kumeza dawa hovyo pasipokujua wanasumbuliwa na tatizo au ugonjwa gani.