Maagizo saba Rais Samia nishati safi

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 09:29 AM May 09 2024
Rais Samia Suluhu Hassan.
Picha: Maktaba
Rais Samia Suluhu Hassan.

RAIS Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo saba kuhusu nishati safi ikiwamo Wizara ya Nishati kuhakikisha inaweka mazingira mazuri kwa wadau wa sekta binafsi kufika vijijini na kuweka vituo vya kujazia gesi.

Amesema kuna Watanzania wengi wanapatiwa mitungi ya gesi, lakini baada ya kutumia na kuisha hawana mahali pa kujazia.

Rais Samia pia amemtaka Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Selemani Jafo, kuandaa katazo kwa taasisi zote zinazohudumia watu zaidi ya 100, kuwa ni marufuku kutumia kuni kupikia.

Amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia ni mahitaji ya lazima na siyo hanasa.

Akizungumza jana mkoani Dar es Salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa mkakati wa taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia ya 2024 -2034, Rais Samia ameitaka Wizara ya Nishati, kufikisha mkakati huo kwa njia rasmi, kwa wadau wote muhimu, pamoja na kutafsiriwa kwa lugha mbili Kiswahili na Kingereza, ili wananchi wote waweze kuutumia.

“Pia wizara ikae na wadau husika serikalini ikiwamo sekta ya fedha na mipango na binafsi kubaini maeneo ambayo yakifanyiwa kazi yataongeza upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa gharama himilivu, pamoja na kushirikiana na wadau muhimu kuhakikisha kunakuwa na mfuko wa kuendeleza nishati safi ya kupikia ifikapo 2025.

“Kwa pamoja tutajua jinsi ya kutafuta fedha zitakazoingia kwenye mfuko, pia tuone namna nishati safi ya kupikia itakavyoweza kutokea kwenye dira ya taifa ya mwaka 2050.

“Na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) iboreshe mikataba inayoingia na wakuu wa mikoa na wilaya ili kuongeza kifungu cha matumizi ya nishati safi katika upimaji wa utendaji kazi wao,” amesema.

Pia amebainisha kuwa watathmini athari za kimazingira, kiuchumi na kiafya ni wazi kwamba, ukosefu wa nishati safi ya kupikia inarudisha nyuma jitihada za maendeleo ya nchi.

Amesema safari hiyo haiwezi kuwa kubwa ikiwa asilimia 90 ya wananchi bado wanatumia nishati isiyo rafiki.

Rais Samia amesema serikali inajukumu la kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu nishati safi ya kupikia na kutunga sera nzuri wezeshi ili kufikia malengo ya mkakati huo.

“Katika hili Wizara ya Nishati watatuongoza kuhakikisha nishati safi ya kupikia inapatikana kwa uhakika na kwa bei inayohimilika kwa wananchi. “Sekta binafsi tunaitarajia pamoja na kuongeza uwekezaji, na upatikanaji wa nishati safi sehemu mbalimbali nchini, watuletee pia teknolojia itakayowezesha wananchi kupata nishati hiyo kadri ya uwezo wao.

“Kwa mfano kulipia kadri anavyotumia kama inavyofanyia katika umeme au maj. Moja ya mikutano ya mazingira niliyowahi kuhudhuria nilishaikuta hii teknolojia, ninaomba wenye utaalamu huo watafutwe, kama wapo wajitokeze tufanye nao kazi katika eneo hilo,” amesema.

Rais Samia amesema ni lazima wakuze na kuvutia uwekezaji zaidi katika uzalishaji wa majiko banifu, umeme na kuhamasisha uzalishaji wa vifaa vya gesi asilia nchini, akibainisha kuwa hatua hizo zitasaidia kupunguza gharama za nishati.

Aidha, amesema kuna haja serikali na sekta binafsi kukutana ili kuangalia namna ya kuongeza ubunifu katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazochangia matumizi madogo ya nishati safi, pamoja na kuangalia nani aliyeweza kuendelea kuongeza matumizi ya umeme kwa ajili ya kupikia.

“Lazima watu wabadilike, akiona mtungi wa gesi anasema ugali nitausongaje, maharage nitayapikaje, ubwabwa matandu nitayapatia wapi, lakini ladha ya chakula nikipikia kuni na hii ni tofauti.

“Hivyo ni vya kufikirika na namna tunavyokwenda, tukiendekeza hayo yatatupa hasara zaidi, ni lazima tuyaepuke, tubadilike kifikra,” amesisitiza na kutoa rai kwa wananchi kuendelea kupanda miti ili kulinda mazingira na kufidia uharibifu ambao ulishafanyika.

Amesema kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ndani ya miaka 10 haitakuwa kazi rahisi, lakini kwa kuwa wote wana nia njema, watatimiza adhma hiyo.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amesema watahakikisha wanazuia matumizi ya nishati isiyokuwa safi katika maeneo yote nchini, pamoja na kusimamia ipasavyo mkakati huo ili kuleta matokea ya haraka na kupunguza athari za kimazingira na afya zinazotokana na matumizi ya nishati chafu.