Majaliwa aagiza wadau afya kuboresha afya ya mama

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 09:23 AM May 06 2024
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa.
PICHA: MAKTABA
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewaagiza watumishi wa Wizara ya Afya, wadau wa afya na jamii kushirikiana kuboresha huduma ya afya ya mama nchini.

Majaliwa alitoa maagizo hayo katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani jijini Dar Salaam.

Amesema ni muhimu watumishi hao wakashirikiana na vyama vya kitaaluma kama Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA) kwa kuwa wadau muhimu katika afya nchini.

Amesema huduma za ukunga zinahitaji ushirikiano kati ya wadau hao na jamii kwa kuzingatia kuwa kila aliyezaliwa amepitia mkononi mwa wakunga.

"Hivyo ninaagiza kwamba shirikianeni ili kuboresha huduma ya afya kwa ajili ya kupunguza idadi ya vifo vinavyotokana na uzazi," amesema Majaliwa.

Amefafanua kuwa kutokana na huduma zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau, vifo wakati wa kujifungua, vimepungua kutoka 558 mwaka 2015/16 hadi kufikia 104 mwaka 2022.

“Hiyo yote imetokana na huduma nzuri ambazo zinaendelea kutolewa na serikali katika jamii, hivyo tuendelee kushirikiana," amesema Waziri Mkuu.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Rais wa TAMA, Beatrice Mwilike, ameiomba serikali kutengeneza mfumo wa kuwezesha wakunga kuhudumia wajawazito wakati wa kujifungua na watoto wachanga.

Amesema wakunga wanatakiwa kujengewa uelewa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, athari zake kwenye afya ya uzazi, jinsi ya kuwahudumia waathirika na kuzuia matatizo yatokanayo na athari hizo.

"Tunaomba serikali kutambua taaluma ya ukunga katika utumishi wa umma kwani wahitimu bado wanaajiriwa kwa cheo cha Ofisa Muuguzi kitendo kinachopunguza morali wa kufanya kazi," amesema Beatrice.

Naibu Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), Tanzania, Melissa Barret, amesema shirika hilo limezindua mradi wa 'Thamini uzazi salama'.

Kwa mujibu wa Melissa, mradi huo wa miaka saba utatekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam na Shinyanga.

"Mradi huu unalenga kuboresha na kuwezesha wakunga wataalamu Tanzania, ambao ni baina ya Serikali ya Tanzania Umoja wa Mataifa (UN)na Serikali ya Canada," amesema.

Amesema ni muhimu kuwa na wakunga wataalamu na ndio sababu wameamua kuendesha mradi huo na wanatarajia kuelimisha wakunga ili waweze kuboresha kazi zao na kuwa na uzazi salama zaidi.

"Ni ukweli usiopingika kuwa wakunga wataalamu ni watu wa muhimu katika afya ya mama na mtoto ili kupunguza vifo vya wajawazito na watoto," amesema.

Mwakilishi wa Balozi wa Canada nchini, Hellen Fytche, amesema nchi yake ina ushirikiano mzuri ya Serikali ya Tanzania na ni mdau mkubwa wa afya ya mama na mtoto na kwamba ndio sababu imetoka Dola bilioni 12 ili kufanikisha mradi huo.

 "Mkunga mtaalamu ni nguzo ya afya ya mama na mtoto, hivyo ninaamini mradi huu utasaidia kuwaongezea ujuzi wakunga na kufanya kazi yao kwa weledi zaidi," amesema Fytche.