Malecela awapigia chapuo vijana kuajiriwa kwa wingi

By Peter Mkwavila , Nipashe
Published at 02:54 PM Apr 18 2024
Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela akiwaonyesha waandishi wa habari zao la mtama, walipotembelea shambani kwake katika kijiji cha Chamwino, wilaya ya Chamwino, mkoani Dodoma, kwa ajili ya kujifunza.
PICHA: PETER MKWAVILA
Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela akiwaonyesha waandishi wa habari zao la mtama, walipotembelea shambani kwake katika kijiji cha Chamwino, wilaya ya Chamwino, mkoani Dodoma, kwa ajili ya kujifunza.

WAZIRI Mkuu mstaafu, John Malecela amesema Tanzania hivi sasa inahitajika kutoa nafasi nyingi za uongozi kwa vijana ukinzingatia kuwa karibu asilimia 60 walio wengi ni kati ya wenye umri wa miaka 18 hadi 40

Amesema kuwa, kutokana na wingi huo wa vijana wanatakiwa kupatiwa nafasi za uongozi ili kuleta mabadiliko zaidi ya maendeleo ndani ya nchi.

Malecela amesema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari waliomtembelea kwenye shamba lake lililopo katika Kijiji cha Chamwino.

Amesema hivi sasa kwa zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania wengi wao ni vijana kati ya umri wa miaka 18 hadi 49, nchi inahitaji kuongozwa na wao na wakipewa wataongoza vizuri.

"Tusiwe na mashaka nao hawa vijana wetu naamini wakipewa nafasi hizo wataongoza na kusimamia vema, kinachotakiwa ni kuwaamini na wanaweza kuongoza vizuri kama viongozi wengine waliopewa dhamana ya kuongoza na kusimamia ambao tunao kwenye nyanja mbalimbali za uongozi," amesema. 

Amewataka vijana kuchangamkia fursa ya kujiajiri kwenye sekta ya kilimo, badala ya kubaki kwenye manun'guniko ya kukosa ajira wakati ardhi ya kutosha kwenye halmashauri ipo.

Aidha, wasikate tamaa kwa ajili ya kukosa ajira serikalini kwa kuwa suala hilo lipo karibu ulimwenguni kote, badala ya kunung'unika wanatakiwa kuwa na mawazo ya kuibua miradi kwenye sekta ya kilimo.

Amesema bado serikali inaendelea kuwakumbuka na kuwajali kuwapatia ajira sekta mbalimbali, kinachohitajika kwa upande wao pia kubuni miradi itakayowafanya kuondokana na kufikiria kuajiriwa.

"Niwasihi vijana wangu kuwa ajira kubwa hapa nchini ipo kwenye sekta ya kilimo, niwaombe na kuwashauri wachangamkie fursa hiyo muhimu, badala ya kukaa na kunung'unika na kusubiri ajira za serikalini," amesisitiza.

Aidha, waendelea kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na utendaji wake, ambao umeonyesha ndani ya uongozi wake umeleta mabadiliko makubwa na kuipaisha nchi kwenye nyanja mbalimbali ya miundombinu.