Matarajio ya Samia kwa watahiniwa kidato VI

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 11:14 AM May 07 2024
Wanafunzi wakifanya mitihani.
PICHA: MAKTABA
Wanafunzi wakifanya mitihani.

RAIS Samia Suluhu Hassan, amewaeleza watahiniwa wa kidato cha sita walioanza mitihani yao jana kuwa, anatarajia kuona vipawa, juhudi na kujituma ili kuleta mchango wao katika maendeleo ya nchi siku zijazo.

Katika ukurasa wake wa Instagramu, Rais Samia ametoa ahadi yake kwa wanafunzi hao kuwa ataendelea kufanyakazi, kupanga na kutekeleza mipango na sera 

zitakazowawezesha kutimiza nia ya kuwa na wananchi wenye mchango mkubwa kwa jamii na taifa.

"Ikiwamo kuongeza fungu kwa wanafunzi zaidi kupata mikopo ya elimu ya juu na kuboresha sera na mazingira ya kukua kwa sekta binafsi ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa katika kuzalisha ajira nchini," amesema Rais Samia katika ukurasa huo.

Aidha, amewaombea watahiniwa kwa Mwenyezi Mungu wafanikishe katika hatua hiyo kwa mafanikio na kila jema katika hatua zinazofuata.

"Nina imani kuwa mmetumia muda wenu shuleni kujiandaa vyema, hasa baada ya serikali kuamua kufuta ada kwa kidato cha kwanza hadi sita, kujenga na kuboresha shule zaidi.

"Ujenzi wa mabweni sehemu ambazo wanafunzi hasa wa kike walikuwa kwenye mazingira hatarishi na kuongeza bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

"Uamuzi huu umeleta nafuu na faraja katika familia nyingi na ongezeko la watahiniwa zaidi kutoka 106,883 mwaka 2023 hadi 113,504 mnaoanza mitihani leo (jana), amesema.

Juzi Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Dk. Said Mohamed, ametangaza kuanza kwa mitihani ya kidato cha sita kuanzia jana hadi Mei 24, 2024 na ualimu itakayomalizika Mei 20.

Katika mitihani hiyo watahiniwa wa shule waliosajiliwa, wavulana ni 57,378 sawa na asilimia 54.9 na wasichana ni 47,071 sawa na asilimia 45.1.

Watahiniwa wenye mahitaji maalum ni 232 na kati yao, 201 ni wenye uoni hafifu, 16 ni wasioona na 15 ni wenye ulemavu wa viungo vya mwili.

Aidha, kati ya watahiniwa wa kujitegemea 9,055 waliosajiliwa, wavulana ni 5,515 sawa na asilimia 60.91 na wasichana ni 3,540 sawa na asilimia 39.09. 

Watahiniwa wa kujitegemea wenye mahitaji maalum wako watatu ambao wote ni wenye uoni hafifu.