Mikoa yahadharishwa athari kimbunga ‘Hidaya’

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:32 AM May 04 2024
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama.

SERIKALI imeagiza mamlaka za mikoa zitakazokumbwa na athari za kimbunga cha Hidaya kuendelea kuchukua tahadhari za kutosha ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kuhusu mwenendo wake, ili hatua stahiki zichukuliwe iwapo dalili zilizobainishwa zikijitokeza.

Tahadhari hiyo imetolewa baada ya kasi ya kimbunga hicho kuendelea kusogea Pwani ya Tanzania, huku kikitarajiwa kuendelea mpaka Mei 6, mwaka huu.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama,  alitoa tahadhari hiyo jana bungeni jijini Dodoma.

Mhagama alisema kwa mujibu wa taarifa iliyotewa jana na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), kimbunga hicho ambacho kinachokuja uelekeo wa Mashariki mwa Pwani ya Tanzania, kimeendelea kuimarika na kusogea eneo la pwani mwa Tanzania.

Alisema hadi kufikia saa tisa usiku jana, kilikuwa kimeimarika zaidi na kufikia hadhi ya kimbunga kamili kikiwa umbali wa km 401 Mashariki mwa Pwani ya Mtwara.

Waziri Mhagama alizitaka taasisi mbalimbali nchini zikiwamo kamati za usimamizi wa maafa ngazi za mikoa, wilaya, kata, mitaa na vijiji kuendelea kuchukua tahadhari na kufuatilia kwa karibu taarifa za mamlaka ya hali ya hewa.

 “Wananchi wanaoishi katika maeneo yaliyotajwa na wote wanaojihusisha hasa na shughuli mbambali baharini, wanashauriwa kuchukua tahadhari kubwa ikiwa ni pamoja na kuendelea kufuatilia taarifa za utabiri kutoka mamlaka husika,” alisisitiza.

Mhagama alisema katika kipindi hiki, kimbunga Hidaya kimeendelea kuimarika zaidi huku kasi ya upepo ikiongezeka hadi kufikia kilometa 130 kwa saa na mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa baharini bado inaonyesha uwezekano mkubwa wa kimbuka  kusalia katika hadhi ya kimbunga kamili hadi kufikia saa 12 zijazo huku kikiimarika.

Alisema kibunga hicho kitaendelea kusogea kabisa katika Pwani ya Tanzania ambapo kinatarajiwa kuendelea kuwapo hadi Mei 6, mwaka huu, na kupungua nguvu baada ya tarehe hiyo.

Kuwapo wa kimbunga hicho nchini, alisema kunatarajiwa kutawaliwa na kuathiri mifumo ya hali ya hewa ikiwa ni pamoja na kuathiri vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali katika baadhi ya maeneo ya mikoa.

Mhagama aliitaja mikoa hiyo ni Mtwara, Lindi, Pwani pamoja na Visiwa vya Mafia, Dar es Salaam, Tanga, Morogoro na upande wa pili wa muunga katika maeneo ya Unguja na Pemba.

Alisema kutakuwapo kwa vipindi vya mvua nyepesi na upepo wa wastani ambavyo tayari vimeanza kujitokeza katika maeneo ya Mtwara, huku ongezeko la mvua na upepo mkali unaoambatana na mawimbi makubwa, vikitarajiwa kusambaa katika maeneo mengi ya ukanda wa pwani kuelekea leo hadi Jumatatu ijayo (Mei 6, mwaka huu).

Pia aliziomba taasisi za dini, viongozi pamoja na wananchi kuendelea kumuomba Mungu kadri ya imani zao ili ikiwezeka nchi iepukane na janga hilo hatari.

“Mamlaka ya Hali ya Hewa inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa kimbunga Hidaya pamoja na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila baada ya masaa matatu, mara kwa mara pale itakapobidi,” alisema.

Baadaye, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi, alisema kasi ya kimbunga hicho hadi jana jioni iliongeza hadi kufikia km 342 kutoka Pwani ya Mtwara.

IMEANDALIWA na Vitus Audax na Paul Mabeja (DODOMA)