Mpango wa Samia kupunguza vifo watoto wachanga kuanza

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 10:06 AM May 07 2024
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.
PICHA: MAKTABA
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.

SERIKALI inakusudia kuanzisha wodi maalum za watoto wachanga (NCU) katika hospitali za halmashauri ili kuboresha huduma na kupunguza vifo vya kundi hilo kutoka vifo 24 kati ya vizazi 1,000 kwa sasa.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, katika hafla ya uzinduzi wa Mpango Kabambe wa Madaktari Bingwa wa Dk. Samia uliofanyika katika Mkoa wa Iringa.

Katika mpango huo madaktari bingwa watasambazwa katika hospitali za ngazi ya halmashauri na kukaa kwa siku tano wakiwahudumia wagonjwa mbalimbali, ikiwa ni mpango wa Rais Samia wa kuboresha huduma ya afya nchini.

Waziri Ummy amesema kupitia mpango huo wanalenga kusaidia hospitali katika ngazi za halmashauri kuanzisha na kuimarisha wodi maalum za watoto wachanga ili kuokoa maisha ya watoto hao nchini.

Amewaelekeza madaktari bingwa wa watoto wachanga waliokuwa katika mpango huo kuhakikisha wanaboresha huduma hizo katika hospitali watakazokwenda kuhudumia ili mpaka watakapoziacha ziwe na huduma zilizoimarika.

“Nasisitiza tena kwamba, sambamba na utoaji huduma na kujenga uwezo wa watoa huduma wetu, madaktari bingwa saidieni uanzishaji na kuimarisha utendaji wa NCU kwa kuwa katika mpango huu mtafikia hospitali zote za halmashauri,” amesema.

Amesema nchi hiyo bado haijafanya vizuri katika kupunguza vifo vya watoto wachanga kwani takwimu zinaonyesha kuwa vimepungua kwa asilimia nne pekee, kutoka 25 katika kila vizazi hai 1,000 hadi 24 katika vizazi 1,000.

Amesema serikali kwa kushirikiana na wadau wakiwekeza vizuri katika huduma ya watoto wachanga wanaweza kupunguza vifo hadi asilimia 50.

“Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza pasi na shaka kwamba tukiwekeza kwenye wodi za watoto wachanga tutapunguza vifo vya watoto hao kwa zaidi ya asilimia 50, ndio maana tumeanzisha mpango huu kabambe wa madakatari bingwa ili pia tukaweke msukumo wa kuanzishwa wodi za watoto wachanga,” amesema.

Mpango huo pia unakusudia kuboresha huduma nyingine za afya nchini ikiwamo uzazi na wanawake, upasuaji, magonjwa ya ndani, huduma ya ganzi na usingizi hivyo madaktari bingwa katika maeneo hayo watazunguka katika halmashauri zote 184 nchini kutoa huduma.

Aidha, amesema lengo la mpango huo ni kuwajengea uwezo watoa huduma katika maeneo ya kazi, ili kuimarisha utambuzi wa magonjwa, matibabu ya magonjwa, upasuaji na rufani kwa wagonjwa ngazi ya hospitali ya halmashauri.


 â€śRais Samia ameandika rekodi duniani na barani Afrika ya kupunguza vifo vya wajawazito kwa asilimia 80. Kutoka vifo 556 katika kila vizazi laki moja hadi 104 katika kila vizazi,” amesema .

Amesema jumla ya madaktari 95 wapo katika kanda hiyo inayohusisha mikoa ya Iringa, Njombe na Ruvuma na watakaa kwa siku tano kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa.

Aidha, serikali inaendelea kuboresha mfumo wa bima ya afya ili kuhakikisha wananchi wote wa kijijini na mijini wanapata huduma bora za afya na katika hilo itasimama kwenye mstari kuhakikisha sheria na kanuni za bima ya afya zinazingatiwa katika uendeshaji wa mfuko huo.

Pia wataanza maandalizi ya Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ikiwamo kubainisha wasio na uwezo, ili utekelezaji wake utakapoanza kusiwepo malalamiko ya mtu kuachwa.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Kheri James, amemshukuru Rais Samia kwa kuanzisha mpango huo kwa kuwa utawasaidia wananchi kupata huduma ambayo walilazimika kutumia gharama kubwa na kutembea umbali mrefu ili kuifuata.

“Tunafahamu daktari bingwa gharama yake ya huduma ni kubwa, upatikanaji wake ni mgumu, lakini mmeacha fedha, mmeacha fursa mmeamua kuja kuwahangaikia Watanzania wenzenu hawa,” amesema.

Amewasihi wananchi wa mkoa huo kutumia fursa hiyo kukutana na madaktari katika hospitali zao za wilaya ili kupata huduma waliokuwa wanaikusudia.

Amewaagiza pia viongozi wa wilaya hiyo ikiwamo wabunge, wenyeviti wa halmashauri, madiwani kuwahamasisha wananchi wao kwenda kupata huduma hiyo ambayo walikuwa wakitembea muda mrefu kuifuata.

Mkurugenzi Msaidizi wa huduma za mama na mtoto, Dk. Felix Bundala, amesema katika siku tano walizohudumia madakatari hao mikoa ya Tanga, Songea na Geita wamefikiwa wateja 6,381.

“Kati ya wateja 6,381 walioonwa, waliofanyiwa upasuaji ni 166 sawa na asilimia 3 waliopewa rufani ni 42 ambao ni sawa na mtu mmoja katika watu 100 amepata rufani,” amesema Dk. Bundala.