Mwenge wa Uhuru wazindua mradi wa maji Ruvu Stesheni, kaya 164 kunufaika

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 05:21 PM May 02 2024
 Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024, Godfrey Eliakim Mnzava akizundua mradi wa maji.
Picha: Julieth Mkireri
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024, Godfrey Eliakim Mnzava akizundua mradi wa maji.

MWENGE wa Uhuru 2024, umemtua Mama ndoo kichwani kwa kuzindua Mradi wa Maji katika Kijiji cha Ruvu Stesheni, mradi ambao utawezesha wananchi kupata huduma ndani ya nusu saa kwa umbali chini ya mita 400.

Mradi huo ambao umesimamiwa na wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) unakwenda kunufaisha kaya zaidi ya 164.

Akizindua mradi huo Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024, Godfrey Eliakim Mnzava amesema ameridhishwa na ujenzi wa mradi huo ambao unakwenda kuondoa kero ya maji  na kuachana kutumia mji ya Mto Ruvu ambayo hayakuwa safi na salama.

Awali akiwasilisha taarifa ya mradi huo Meneja wa RUWASA Mhandisi Debora Kanyika amesema mradi huo umetekelezwa kwa fedha za mfuko wa Taifa wa maji (NWF) kwa gharama ya Sh.milioni 328.

Mhandisi Kanyika amesema chanzo cha maji cha mradi huo ni kisima kifupi chenye uwezo wa kutoa lita 11,820 Kwa saa na kina urefu wa mita 43.

Amesema kabla ya kujengwa mradi huo kaya 81 zilikuwa zinapata maji na sasa  kaya 164 zinakwenda kunufaika kati ya hizo 33 zimeunganishiwa maji nyumbani.

Kwa mujibu wa Mhandisi Kanyika mradi huo umesanifiwa kuweza kutoa huduma hadi kufikia kaya 520 ifikapo 2042.

Akizungumza Kijijini hapo Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji Ruvu Stesheni Ally Said amesema uwepo wa mradi huo unasaidia kuondokana na hatari ya kuliwa na mambo ambapo wapo wananchi wamebaki na majeraha hadi sasa yaliyotokana na kufuata maji mto Ruvu.

Mery Stanphod mkazi wa Kijiji hicho amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Awamu ya Sita Dk. Samia Suhulu Hassan  kwa kutoa fedha za kutekeleza mradi huo ambapo anasema awali walikuwa wakisumbuliwa na magonjwa ya tumbo kutokana na kutumia maji ambayo hayakuwa safi na salama.