RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameihakikishia Serikali ya Saudi Arabia ushirikiano mzuri uliopo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hasa kwenye miradi mbalimbali ya Maendeleo.
Taarifa hiyo imetolewa na Idara ya Mawasiliano, Ikulu Zanzibar imesema Rais Mwinyi amesema hayo wakati akizungumza na Balozi wa Saudi Arabia nchini, Yahya Ahmad Okeish, na ujumbe wake, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano ulioko baina ya nchi mbili hizo.
Dk. Mwinyi amesema SMZ ni mnufaika mkubwa wa mifuko ya Saudia na Kuwait katika miradi yake ya maendeleo kupitia ushirikiano mzuri ulioko baina ya mataifa hayo.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi ameishukuru na kuipongeza serikali ya Saudi Arabia kwa ushirikiano wake na Tanzania hususan kuipatia zawadi mbalimbali inazozituma kwa watu wa Zanzibar zikiwamo tende wakati wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Katika salamu zake kwa Tanzania, Balozi Okeish amepongeza mafanikio makubwa yaliyofikiwa na taifa hili kwa kutimiza miaka 60 ya Muungano wake baina ya Tanganyika na Zanzibar, sambamba na kuuombea mafanikio zaidi.
Pia Balozi Okeish amesifu ushirikiano wa diplomasia ulioko baina ya nchi hizo mbili ikiwamo Zanzibar pamoja na tamaduni.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED