"Nyongeza ya siku za likizo ya uzazi wanaojifungua watoto njiti italeta tija sehemu za kazi"

By Frank Monyo , Nipashe
Published at 10:13 PM May 07 2024
Makamu Mwenyekiti wa TUGHE Taifa, Dk. Jane Madete akizungunza na waandishi wa habari Leo.
Picha: Mpigapicha Wetu
Makamu Mwenyekiti wa TUGHE Taifa, Dk. Jane Madete akizungunza na waandishi wa habari Leo.

Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) kimesema kuwa kimefurahishwa na Uamuzi wa Serikali wa kukubali ombi lililokuwa likiwasilishwa na Chama hicho la kuongeza Siku ya Likizo ya uzazi kwa Wafanyakazi Wanawake wanaojifungua watoto njiti kama ilivyotangazwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Philip Mpango alipokuwa Mgeni Rasmi wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani-Mei Mosi Kitaifa jijini Arusha.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo katika Tawi la TUGHE Hospitali ya Rufaa ya Temeke Jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa TUGHE Taifa, Dk. Jane Madete amesema kuwa Wafanyakazi wanawake waanaojifungua watoto njiti wanapitia changamoto mbalimbali ikiwemo za kiafya, hivyo wanahitaji kupata muda mwingi wa kupumzika na pia kumuhudumia mtoto toka katika kipindi cha uangalizi hadi wanaporuhusiwa kutoka hospitalini Ndiyo maana Chama cha TUGHE kwa kutambua hilo kiliamua kubeba ajenda hiyo na kuiomba Serikali iweze kuongeza siku za likizo ya uzazi ili kuleta tija sehemu za kazi.

“Kufuatia uamuzi huu tunaiomba serikali sasa ianze mchakato wa kufanya marekebisho katika Sheria ya Ajira na Mahusiano kazini ambayo kwa sasa  imekuwa ikitoa siku 84 kwa wanawake wanaojifungua mtoto mmoja na pia siku 100 kwa wanaojifungua zaidi ya mtoto mmoja. TUGHE tupo tayari kushiriki kikamilifu katika hatua zote za kuhakikisha uamuzi huu unaingia katika sheria hii” amesema Dk. Madete

Kwa upande wa Sekta Binafsi, TUGHE imewaomba Waajiri nchini katika mikataba yao ya hali bora kuweka kipingele cha kuongeza muda kwa siku za likizo ya uzazi kwa wanaojifungua watoto njiti kama ambavyo mwishoni mwa mwaka jana 2023 Chama cha TUGHE waliweka kipengele hicho katika Mkataba wake wa Hali Bora na kuwa Chama cha kwanza cha Wafanyakazi Nchini kufanya hivyo katika Mkataba wake wa hali bora.