Polisi Morogoro yakanusha taarifa za wanafunzi kutekwa

By Christina Haule , Nipashe
Published at 04:01 PM May 08 2024
Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, SACP Alex Mkama.
Picha: Maktaba
Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, SACP Alex Mkama.

JESHI la Polisi mkoani Morogoro, linamsaka mtu au watu waliotuma na wanaoendelea kusambaza taarifa za uzushi zinazodai kutekwa kwa watoto 12 wa shule ya awali ya kanisa la Kiinjili la Kilutheri iliyopo katika Tarafa ya Mahenge Wilayani Ulanga.

Akizungumza na vyombo vya Habari, Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, SACP Alex Mkama, amesema mwanzoni mwa mwezi Aprili mwaka huu taarifa zilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii zikidai kuwa watoto hao walitekwa na mwanamke mmoja na kuwapakia kwenye gari na kudai kuwa mwanamke huyo tayari ameshamakamatwa na jeshi la polisi jambo ambalo sio kweli.

Kamanda Mkama amesema taarifa hizo ni za uongo hivyo baada kuona zinasambaa walilazimika kufanya uchunguzi hadi kwenye shule husika na kubaini kuwa siku ya tukio lilipoanza kusambazwa watoto hao walikuwa 44 darasani kati ya wanafunzi 46 waliopo kwenye kituo hicho.

Hivyo amewataka wananchi kuzipuuza taarifa hizo ambazo ni za uzushi na zilipikwa ili kuchafua na kuleta taharuki kwa lengo la kuvuruga hali ya usalama na amani ya wilaya na mkoa kwa ujumla.

Aidha, Jeshi la Polisi linawataka wananchi kuacha tabia ya kutuma taarifa za kuzusha na kuleta taharuki kwenye mitandao ya kijamii kwa sababu kufanya hivyo ni kosa na atakayebainika atachukuliwa hatua za kisheria.