Samia mgeni rasmi Red Cross inapotimiza miaka 62 ya kazi

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 03:06 PM May 07 2024
Watumishi wa Red Cross Lucy Pande (katikati), Alfred Mwanjali (kulia) na Seki Kasuga (kushoto), walikizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo.
PICHA: SABATO KASIKA
Watumishi wa Red Cross Lucy Pande (katikati), Alfred Mwanjali (kulia) na Seki Kasuga (kushoto), walikizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo.

RAIS Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe za Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania (Red Cross), kutimiza miaka 62 ya huduma zake kwa jamii nchini.

Katibu mkuu wa chama hicho, Lucy Pande ameyasema hayo, jijini Dar es Salaam, leo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya sherehe hizo zitakazofanyika Mei 11, jijini Dodoma.

"Tumemualika Rais Samia Suluhu Hassan na amekubali mwaliko wetu, hivyo ninawaalika pia Watanzania wengine kuungana nasi katika sherehe hizo za kutimiza miaka 62 ya huduma zetu nchini," amesema Lucy.

Lucy amesema, sherehe hizo zitaambatana na matukio mbalimbali akiwamo kuwazaidia wafanyakazi wa kujitolea, na kwamba nguvu za chama hicho ziko kwa wafanyakazi hao.

"Mkoa ambao wafanyakazi wa kujitolea wameingiza watu wengi kuwa wanachama wetu, mkoa ambao wamekusanya damu nyingi kwa miaka mitano ambayo tumeingia madarakani lakini pia mkoa ambao umepanda miti kutunza mazingira, wote hao tutawazawadia," amesema.

Amesema anaalika Watanzania kuhudhuria sherehe hizo, ili kushuhudia kazi zinazofanywa na chama hicho zikiwamo na kusaidia na kuokoa watu katika majanga yakiwamo ya mafuriko, ukame na ajali.

Kiongozi huyo ametaja baadhi ya mafanikio ya chama hicho, amesema katika kipindi cha miaka mitano ambacho ameingia madarakani, wafanyakazi wa kujitolea walikuwa 3,000 na kwamba sasa ni 600,000.

"Wakati tunaingia madarakani, kulikuwa na wanachama 9,000, sasa wameongezeka hadi kufikia 800,000, ni mojawapo ya mafanikio kwetu mbali na huduma za kibinadamu tunazotoa katika jamii," amesema.

Mbali na mafaniko hayo, Katibu Mkuu amesema, chama kwa sasa kina ofisi katika mikoa 19, na kwamba, kinajipanga kuwa na ofisi nchi nzima kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

"Vilevile, Red Cross ina timu ya uokoaji nchi nzima kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa, ndio maana yakitokea maafa sisi huwa ni wa kwanza kufika kutoa msaada," amesma.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maafa wa Red Cross, Alfred Mwanjali, amesma, katika kipindi cha miaka mitano ambacho wameingia madarakani, wamefanikiwa kukusanya uniti 74,000 za damu.