Tanzania yaahidi kuisaidia Somalia kurejesha amani

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 09:18 AM Apr 28 2024
Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na Rais wa Jamhuri ya Somalia, Hassan Sheikh Mohamud.
PICHA: IKULU
Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na Rais wa Jamhuri ya Somalia, Hassan Sheikh Mohamud.

RAIS Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Somalia, Hassan Sheikh Mohamud, wamefanya mazungumzo na kukubaliana kuendelea kushirikiana katika nyanja mbalimbali, huku Tanzania ikiahidi kuunga mkono jitihada za kuirejeshea amani nchi hiyo.

Marais hao wamekubaliana na mawaziri wa kisekta na wataalam wakiratibiwa na mawaziri wa mambo ya nje, wakutane wazungumze halafu waibue maeneo ya kushirikiana.

Wakizungumza baada ya mazungumzo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam jana, maraisi hao pia walikubalinana kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kuwa na mfumo rasmi wa kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo.

Rais Mohamud ambaye yuko nchini kwa ziara ya kikazi, akiambatana na ujumbe wake, alikuwa miongoni mwa marais walioshiriki sherehe za miaka 60 ya Muungano wa Tanzania.

“Tumemshukuru sana kwa kukubali mwaliko wetu wa kufanya ziara ya kiserikali hapa kwetu, ni ziara ya kwanza ya kiserikali hapa nchini tangu aingie madarakani na ni ya kwanza ya kiongozi wa kitaifa wa Somalia tangu ijiunge na Jumuiya ya Afrika Mashariki, hii ni ziara ya
kihistoria.

“Tumemshukuru pia, kwa heshima aliyotupa ya kushiriki nasi katika sherehe za miaka 60 ya Muungano,” amesema. 

Rais Samia alisema kadri wanavyokuwa wamoja katika nchi ndivyo wanavyokaribia kujenga mtangamano wa Afrika, hivyo hawana budi kuhakikisha wanadumisha umoja kama walivyodhamiria waasisi wao na wa Umoja wa Afrika.

Amesema katika mazungumzo rasmi ya kiserikali waliyofanya wamegusia maeneo mengi ya kimkakati na muhimu, ukiwamo uhusiano wa kiplomasia licha ya wananchi wa Somalia na Tanzania kuwa na uhusiano na mwingiliano kwa miaka mingi.

“Ziara hii imetupa fursa kujadili uimarishaji wa uhusiano baina ya nchi zetu. Tumeona kuna umuhimu wa kuwa na mfumo rasmi wa kuimarisha uhusiano huo. Ni dhamira yetu kuimarisha mikutano ya mashauriano baina ya nchi zetu mbili, kupitia wadau wetu wa kisekta ndiyo tutaibua maeneo na miradi yenye manufaa kwetu sote,” amesema.

Rais Samia amesema Tanzania inapongeza jitihada za Rais huyo na serikali yake katika kuendeleza vipaumbele vyake vya kitaifa na usimamizi wa ajenda ya usimamizi wa taifa lao, kupitia mashauriano ya kisiasa.

Pia amesema sema wanaipongeza Somalia kwa jitihada zake za kuendelea kurejesha amani na usalama katika nchi yao, kama Ujumbe la Baraza la Amani na Usalama wa Umoja wa Afrika na pia, majukwaa mengine Afrika, hivyo Tanzania itaendelea kuunga mkono jitihada za kurejesha amani .

Amesema serikali ya Somalia imekuwa ikichukua hatua kubwa na za kupongezwa katika masuala ya uchumi na kijamii na wamekubaliana, kuimarisha uhusiano ikiwamo masuala ya kijamii hususani eneo la afya na elimu.

“Tumewapa mwaliko muda wowote wakitaka msaada wetu kwenye afya na elimu waje tuzungumze tutawasaidia. Tumewataka mawaziri wetu wakae wazungumze na waone hayo maeneo.

“Kwa upande wa ushirikiano wa kikanda na kimataifa tumempongeza kwa hatua ya wao kuwa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Tumeahidi ushirikiano wetu katika

kutekeleza masharti mbalimbali ya mtangamano ili manufaa ya hatua hii iwafikie wao na sisi,” amesema.

“Kama mnavyofahamu uhusiano wa mtangamano ndani ya jumuiya yetu unawaweka watu mbele, unasukuma uhusiano wa masoko,” amesema.

Pia amesema wamezungumzia kuhusu umuhimu wa wa nchi hizo kuchukua hatua za makusudi za kukuza zaidi biashara na uwekezaji.
Kadhalika alisema wamemuahidi Rais huyo ushirikiano katika majukwaa ya kikanda na kimataifa ambapo nchi hizo ni wanachama na kwamba, ziara hiyo itawezesha nchi hizo kutumia fursa ipasavyo za kiuchumi na kijamii zitokanazo na jumuiya ya EAC.

Naye, Rais Mohamud amesema ziara hiyo ni heshima kubwa kwao kwani ni sehemu ya kupanua mipaka ya uhusiano baina ya nchi hizo na hivyo, amemshukuru Rais Samia kwa ukaribisho huo. 

Amesema Tanzania imekuwa washirika wa karibu ambao wanataka kuendelea kufanya nao kazi na kushirikiana nao miaka ijayo.

“Tunataka kuendeleza hili kusudi katika msingi ya kuheshimiana na kushirikiana katika maeneo mbalimbali yanayotunufaisha sote. Nimefurahia majadiliano ya leo tumeangalia maeneo ya kimkakati ili kutia nguvu uhusiano wetu. 

“Yale yote ambayo serikali yetu imesema tutayafanya ili kudumisha ushirikiano huu na kujenga mifumo mizuri kusaidiana kiuchumi ,” amesisitiza.

Amesema serikali ya Somalia ina mifumo mbalimbali ya kutengeneza uchumi na wameweza kushusha deni la taifa na kutokana na historia nzuri, Somalia imefanikiwa kuondoa zuio la silaha lililowapo kwa muda mrefu.