Waliopisha ujenzi mradi wa maji wajazwa manoti

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 04:54 PM Apr 18 2024
Waliopisha ujenzi mradi wa maji wapewa fidia.
PICHA: MAKTABA
Waliopisha ujenzi mradi wa maji wapewa fidia.

SERIKALI kupitia Wizara ya Maji imetoa Sh.milioni 444 kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi 97 kutoka vijiji sita wilayani Shinyanga, ambao walitoa maeneo yao kupisha mradi wa maji.

Ofisa Mazingira kutoka Wizara ya Maji, Moses Mgalla ameyasema hayo  wakati wa hafla ya wananchi hao 97 kusaini majendwali ya uthamini, ili waweze kulipwa fidia kupitia benki.

Amesema ulipwaji huo wa fidia umefuata taratibu zote za kisheria.

"Wananchi hao ni kutoka katika vijiji sita ambavyo ni Mwagala, Kolandoto, Ihapa, Kituli, Didia na Mwamakaranga ambao wamepisha maeneo yao kwa ajili ya mradi huu ambao utatekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) na kufadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) kwa ushirikiano na serikali" amesema.

Amesema ulipwaji huo umefikia hatua ya mwisho na wananchi walishirikishwa kuanzia hatua ya kwanza kwa kuainisha maeneo, kufanya uthamini na uhakiki pamoja na kutoa elimu, sasa wanakwenda kuwalipa pesa zao ili kupitisha utekelezaji wa mradi huo.

Amesema kuwa mradi huo unagharimu Euro milioni 76 sawa na Sh. bilioni 200 na unahusisha ujenzi wa mtandao wa majisafi, mitambo minne ya kuchakata tope kinyesi, ukarabati wa mtambo wa kutibu majisafi pamoja na kuijengea uwezo SHUWASA.

baadhi ya wananchi ambao wanalipwa fidia hizo akiwamo Kafula Ngaiwa kutoka Kijiji cha Ihapa, wameishukuru Serikali kwa kuwalipa fidia zao kwa wakati.

Aidha, wametoa wito kwa SHUWASA, kipindi cha utekelezaji wa mradi huo wakumbuke kuwapa ajira vijana wa maeneo yanayopitiwa na mradi.

Mwananchi mwingine, Paul Sitta, amesema wameridhika na fidia ambayo wanalipwa na kwamba wanabariki mradi huo kutekelezwa katika maeneo yao na kuahidi kuilinda miundombinu yake

Amesema: “Naishukuru serikali kwa kuweza kutukamilishia zoezi la kulipwa fidia ya ardhi walioichukua kwa ajili ya matumizi ya utekelezaji wa mradi huu na taratibu zote wamezifuata na tumeridhika na fidia ambayo tunalipwa”.