Wananchi, Polisi kushirikiana kujenga kituo cha polisi Katunguru

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 02:53 PM May 08 2024
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP Wilibroad Mutafungwa.
Picha: Vitus Audax
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP Wilibroad Mutafungwa.

WANANCHI wa Kata na Tarafa ya Katunguru Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, wamejitoa kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa kituo cha Polisi kilichoanzishwa kwa nguvu za wananchi.

Wametoa ahadi hiyo wakati wakizungumza na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP Wilibroad Mutafungwa, alipotembelea na kukagua maendeleo ya kituo hicho.

Akizungumza wakati wa mkutano na wananchi hao, DCP Mutafungwa amewahamasisha kumalizia ujenzi wa kituo hicho kwa wakati ili kiweze kuwahudumia pamoja na wananchi maeneo jirani.

Aidha, ametoa mchango wa Sh. milioni moja na kuahidi kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha kituo hicho kinakamilika na kuanza kutumika.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Katunguru Lukas Lushoshaga amesema ili Polisi wafanye kazi kwa uadilifu wanatakiwa kuwa na mazingira bora ya kufanyia kazi, hivyo kituo hicho kitakapo kamilika kitakuwa msaada kwa wananchi wa Kata ya Katunguru na Kata za jirani.