Wananchi wapewa shime kuchangamkia fursa za uwekezaji nchini

By Frank Monyo , Nipashe
Published at 07:11 AM Apr 28 2024
news
Picha: Frank Monyo
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu) Jenista Mhagama akizungumza wakati wa Kongamano la Nne la Kitaifa la Ushiriki wa Watanzania katika Miradi ya kimkakati na uwekezaji lilofanyika katika ukumbi wa (BoT).

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama ametoa shime kwa Baraza la Uwekezaji wa Wananchi Kiuchumi kwa kushirikiana na sekta binafsi na wadau mbalimbali kutambua mawanda makubwa ya uwekezaji yaliyo katika nchi yetu.

Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza katika Kongamano la Nne la Kitaifa la Ushiriki wa Watanzania katika Miradi ya kimkakati na uwekezaji lilofanyika Jana Aprili, 27, 2024 katika ukumbi wa Benki kuu ya Tanzania (BOT) Jijini Dar es Salaam.

Waziri Mhagama alisema kuwa sekta binafsi na wadau mbalimbali waendelee kutoa mapendekezo kwenye fursa mbalimbali zinazojitokeza za kiuchumi ili kuwezesha utekelezaji wa miradi ya kiuchumi kufikia malengo yaliyopo.

Aliongeza kusema wananchi wa Tanzania wako tayari, wakiongozwa na Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa ameonesha kwa vitendo kwamba yuko tayari hivyo ni vyema kumuunga mkono kwa kufanya kazi ili kujenga uchumi wa Taifa.

Aidha jukwaa hilo litasaidia kujenga uelewa wa pamoja juu ya mafanikio yaliyopatikana na katika uwekezaji na ustawi wake wa kiuchumi.

Waziri aliongezea dhana ya kongamano hilo lenye  kauli Mbiu ya “Wekeza Tanzania kuongeza thamani ya ziada” linatumika kujenga uchumi imara ambao umeshirikisha Watanzania wengi.

“Na itatutengenezea mazingira mazuri ya biashara ambayo yatachochea wananchi wengi katika uwekezaji na ushiriki wao katika kujenga uchumi,"alisema Waziri Mhagama

Baraza la Uwekezaji wa Wananchi Kiuchumi limeingia makubaliano na taasisi ya serikali inayosimamia manunuzi ya umma, katika moja ya kipengele katika sheria ya manunuzi ya umma kinachosisitiza kila asilimia 30 ya manunuzi ya umma ya kila mradi yaende kwa vijana, wanawake wazee na watu wenye ulemavu ambayo ni sehemu ya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.

Kwa upande wake Beng’i Issa Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi wa Kiuchumi (NEEC) amesema moja ya mambo wanayosimamia ni kuangalia kampuni zinazopata kazi kwenye miradi ya kiuchumi na bidhaa zinazouzwa katika miradi hiyo  zinatoka nchini.

Aidha kwenye ajira Baraza la Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi linaangalia ajira za moja kwa moja na ajira ambazo sio za moja kwa moja katika uhaulishaji wa teknolojia kwa kusimamia teknolojia nchini na mipango ya kutoa mafunzo ya kuhaulisha inafanyika.

Akizungumzia kuhusu kongamano alisema kongamano hilo la Nne limelenga katika kujenga uelewa wa pamoja kuhusu ushiriki wa watanzania katika miradi ya kimkakati na uwekezaji unaofanyika hapa nchini pamoja na kushirikishana mafanikio na changamoto zilizopo katika ushiriki wa watanzania katika uwekezaji.