Wataka sheria itungwe kumlinda mtoto wa kiume

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 03:50 PM Apr 30 2024
Sheria itungwe kumlinda mtoto wa kiume.
PICHA: MAKTABA
Sheria itungwe kumlinda mtoto wa kiume.

KUTOKANA na ongezeko la vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwamo ulawiti kwa watoto wa kiume nchini, serikali imeombwa kutunga sheria ya kumlinda mtoto wa kiume kama ambavyo ilifanywa kwa watoto wa kike.

Rai hiyo imetolewa na wadau wa kupinga vitendo vya ukatili kwenye kongamano la kitaifa la wahitimu wa vyuo vikuu waliofadhiliwa masomo yao na Kanisa Katoliki nchini kupitia Programu ya Uongozi wa Kizazi Kijacho (NGLP).

Katibu wa NGLP, Aida Leka akiwasilisha mada ya nafasi ya mtoto wa kiume na changamoto zilizopo kwenye kongamano hilo, amesema watoto wa kiume hivi sasa wanakosa mwongozo kutoka kwa wazazi hali ambayo inasababisha wengi wao kufanyiwa vitendo vya ukatilii.

Amesema pamoja na kukosa mwongozo wa wazazi lakini hivi sasa watoto wa kiume wapo katika mazingira hatarishi zaidi kuliko wa kike, hivyo serikali haina budi kutunga sheria itakayowalinda kama ilivyofanya kwa watoto wa kike.

“Hivi sasa watoto wa kiume wanafanyiwa vitendo vya ukatili nyumbani, shule na mitaani tunaiomba serikali itunge sheria ya kumlinda mtoto wa kiume kama ambavyo ilivyofanya kwa mtoto wa kike,”  amesema.

Aidha,  amesema wazazi pia wanapaswa kuwa mstari wa mbele kulinda watoto wao kwa kuwapa muda wa kuwasikiliza ili waweze kubaini mambo ambayo wanakuwa wakiyapitia mtaani, shuleni na hata nyumbani.

“Wazazi inabidi tubadilike ili kulinda watoto wetu wa kiume kwani hawa wakiharibiwa leo wapi tutapata maaskofu, mapadri kwani mwanaume ndiye mzalishaji wa watoto kwa mujibu wa uumbaji wa Mungu kazi ambayo mwanamke hawezi kufanya,”  amesema.

Kadhalika,  amesema takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya watoto wengi wa kiume wanafanyiwa vitendo vya ukatilii ndani ya nyumba zao na ndugu wa karibu.

“Niwaombe ndugu zangu kama anakuja ndugu yako kutoka kijijini usimlaze na watoto wako kama hana hela ya kulala nyumba ya wageni basi aondoke bora waseme hutaki ndugu lakini siyo kuharibiwa watoto,”  amesema.

Vile vile, amewataka wazazi kuwajengea uwezo watoto wao wa kujiamini na kufanya kazi ili kuondokana na tabia ya tamaa ya kupata fedha za haraka na kujikuta wakiangukia kwenye vitendo vya ushoga na panya road.