Waziri akuta harufu wodini watumishi wakidai stahiki

By Halima Ikunji , Nipashe
Published at 10:36 AM Apr 28 2024
Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel.
PICHA: MAKTABA
Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel.

WAKATI watumishi wa Hospitali ya Rufani Mkoa wa Tabora ya Kitete iliyoko mkoani hapa watumishi wake wakidai hawajalipwa stahiki zao zaidi ya miezi minne, hali ya usafi wa wodi ya wazazi hospitalini hapo si nzuri na kuchangia kuwapo kwa harufu.

Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, amekutana na changamoto hiyo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika hospitali hiyo inayopokea zaidi ya Sh. milioni 267 kila mwezi.

Akiwa katika kikao baina yake na watumishi hao, amebaini changamoto hizo, huku akisema amefika hapo baada ya kuambiwa hospitali inanuka na hilo amejionea alipoingia katika moja ya wodi ya wazazi na kukuta hali ya usafi siyo nzuri.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, watumishi hao wameeleza kukabiliwa na matatizo mbalimbali ambayo hayajashughulikiwa na uongozi kwa muda mrefu, licha ya hospitali hiyo kuingiza mapato kila mwezi, hivyo kuwavunja moyo katika utendaji.

Wamezitaja baadhi ya kero hizo kuwa ni kutolipwa stahiki zao kwa muda mrefu ikiwamo fedha za likizo, matibabu, kutopandishwa vyeo na marupurupu mengine ya kiutendaji. 

Kadhalika wamelalamikia hali ya mazingira ya hospitalini hapo kutoridhisha hususan katika wodi ya wazazi na maeneo mengine, licha ya kuwapo kampuni iliyopewa kandarasi ya kufanya usafi ikidaiwa kutokuwa na uwezo wa kazi na uongozi kuendelea kuitumia.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk. Mark Waziri, amethibitisha kuwapo kwa kero hizo pamoja na hospitali kuendelea na utekelezaji wa jukumu la kutoa huduma za afya kwa weledi kwa jamii.

Hata hivyo, amesema changamoto tajwa zinasababishwa na kupungua kwa fedha za matumizi mengineyo (OC) walizokuwa wanaletewa.

Mhasibu wa hospitali hiyo, Samwel Mgula, amelithibitisha stahiki nyingi za watumishi kutolipwa tangu mwezi Januari hadi sasa kutokana na ukosefu wa fedha, kwa kuwa fedha wanazoletewa kila mwezi hazitoshelezi.

Kutokana na hilo, Naibu Waziri wa Afya, Dk. Mollel amesema serikali inatoa Sh. milioni 267 kila mwezi hospitalini hapo lakini amebaini fedha hizo ziko mifukoni mwa baadhi ya viongozi wa hospitali na kueleza kuwa, hali hiyo halikubaliki, huku akiahidi kuchukua hatua dhidi yao.

“Kwa fedha hizo zote mnazopokea kila mwezi mnashindwaje kuwalipa watumishi stahiki zao na mbaya zaidi wana madai ya muda mrefu, katika hili menejimenti mmeshindwa kazi, tutafanya uamuzi,” amesema.

Dk. Mollel ameongeza kuwa kabla hajafika hospitalini hapo aliambiwa kuwa hospitali inanuka na amelithibitisha hilo ni kweli, kwani ameingia katika moja ya wodi ya wazazi na kukuta hali ya usafi sio nzuri.

Amesema hali ya usafi hospitalini hapo hairidhishi na kuonyesha uongozi umeshindwa kazi na hivyo kuahidi kuwachukulia hatua stahiki watumishi wote wasiowajibika ipasavyo ili kuboresha utoaji huduma.

Naibu Waziri huyo aemelekeza Timu ya Afya ya Mkoa (RHMT) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kusimamia utendaji wa hospitali hiyo wakati wizara ikilifanyia kazi suala hilo na kuahidi kurudi ndani ya wiki mbili ili kutoa uamuzi.

Kaimu Mkuu wa Mkoa huo ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mjini, Deusdedit Katwale, ameahidi kuendelea kusimamia weledi katika suala zima la utoaji huduma za afya katika hospitali hiyo, huku akiahidi kuwa wiki mbili alizowapa watazitumia kufanya marekebisho ya kiutendaji.