WHO, taasisi 11 kuimarisha afya kwa umma

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 09:54 AM May 09 2024
Mwakilishi Mkazi wa WHO Tanzania Dk Charles Moses katikati akisaini makubaliano ya kushirikiana na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Amref Health Afrika -Tanzania Dk Florance Temu.
Picha: Maktaba
Mwakilishi Mkazi wa WHO Tanzania Dk Charles Moses katikati akisaini makubaliano ya kushirikiana na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Amref Health Afrika -Tanzania Dk Florance Temu.

SHIRIKA la Afya Duniani (WHO), limetiliana saini makubaliano na taasisi 11 yakiwamo mashirika yasiyo ya kiserikali na vyuo vikuu, kuimarisha mifumo ya afya kwa umma, kutoa elimu, kinga dhidi ya magonjwa na kufanya utafiti.

Miongoni mwa vyuo hivyo ni Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Baraza la Taifa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Tanzania, Rachel Chagonja, ametia saini pamoja na WHO kwa niaba ya taasisi hizo. 

Chagonja amesema kwamba makubaliano hayo na WHO, yanabainisha nia ya dhati katika kuongeza wigo wa huduma za afya nchini na kuwafikia Watanzania.

Amesema makubaliano hayo ambayo yana malengo yanayowiana na ya shirika hilo kwenye sekta ya afya, kwa kuwajengea uwezo wataalamu wa afya, kufanya utafiti na kuimarisha huduma za afya ngaji ya jamii.

“Tunaishukuru WHO kwa kushirikiana nasi kwenye sekta ya afya Tanzania. Tuitumie fursa hii kwa kufanya kazi pamoja, tukijenga afya na Tanzania itarajiwayo kwa Watanzania,” amesema Chagonja.

Kuhusu manufaa ya makubaliano hayo, Mkuu wa DUCE, Prof. Stephen Maluka, amesema shirika hilo litasaidia wadau wa afya kutekeleza vipaumbele vya afya.

“Makubaliano haya yatasaidia ambao tunatoa elimu na wadau wa afya, kuboresha elimu ya lishe, afya ya uzazi, mama na mtoto pamoja na kinga. Ushirikiano huu, utasaidia kutekeleza vipaumbele vya serikali,” amesema Prof. Maluka.

Makamu Mkuu wa MUHAS, Prof. Apolinary Kamuhabwa, amesema mchakato wa kupatikana taasisi na mashirika 11 ulikuwa wenye ushindani, hivyo walioshinda fursa hiyo watafanya kazi bega kwa bega na WHO, ikiwamo kuandaa miongozo.

Mwakilishi Mkazi wa WHO Tanzania, Dk. Charles Sagoe-Moses, amesema makubaliano hayo yanatambua mchango mkubwa unaofanywa na mashirika na taasisi mbalimbali nchini, kwenye sekta ya afya, kuhakikisha hakuna anayeachwa kando katika afya.

“WHO inatambua thamani na kinachofanywa na taasisi hizi, kuboresha huduma za afya, hususan kwenye ajenda ya Afya Kwa Wote,” amesema.

Amesema makubaliano hayo yatajikita katika kuimarisha mifumo ya afya, kinga dhidi ya magonjwa na Magonjwa Yasiyoambukiza (NCDs), magonjwa ya mlipuko na mtindo bora maisha.