EWURA: Uchachuaji mafuta wapungua hadi asilimia nne

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 06:54 AM May 03 2024
Thobiet Makafu, Ofisa Mwandamizi kutoka EWURA Kanda ya Magharibi, akitoa mada juu ya uchakachuaji mafuta ambapo amesema umepungua hadi asilimia nne.
Picha: Shaban Njia
Thobiet Makafu, Ofisa Mwandamizi kutoka EWURA Kanda ya Magharibi, akitoa mada juu ya uchakachuaji mafuta ambapo amesema umepungua hadi asilimia nne.

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (EWURA) imesema uchakachuaji wa mafuta umepungua hadi kufikia asilimia nne baada ya kuanza kuweka vinasaba katika mafuta yote yanayoingizwa nchini na kusafirishwa katika mikoa mbalimbali.

Ofisa Mwandamizi Uhusiano kwa umma wa EWURA Kanda ya Magharibi Thobiet Makafu ameyabainisha haya leo wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari 30 wa mkoa wa Shinyanga yaliyolenga kuwajengea uelewa zaidi juu udhibiti wa nishati na maji kwa mlaji ili kutomuathiri.

Makafu amesema, mwaka 2007 uchakachuaji wa mafuta ulikuwa kwa asilimia 80 na baada ya kusimamia vema kwa kuongeza udhibiti, kuagiza mafuta kwa pamoja na kuweka vinasababu kwenye mafuta kuanzia bandarini mpaka katika vitu vya mafuta vilivyopo mikoani hatua iliyosaidia kufikia asilimia nne kwa mwaka 2022.

Amesema, awali wafanyabiashara wengi walikuwa wakiagiza mafuta kila mmoja kivyake na uchakachuaji ulikuwa mkubwa lakini baada ya kuweka utaratibu wa kuagiza kwa pamoja tatizo hilo limedhibitiwa na kuwataka wamiliki wa mafuta kuzingatia miongozo ambayo wamekuwa wakipewa ili kuepuka adhabu pale wanapobainika kuyafanya hayo.

Pia amesema, wamekuwa wakitoa leseni kwa mafundi wa umeme waliopo mikoa mbalimbali ili kuondoa vishoka kwa lengo la kudhibiti majanga yanayotaka na nishati ya umeme, baadhi wamekuwa wakiwafuata moja kwa moja katika vyuo vya ufundi na kuelisha umuhimu wake na wale waliojifunza mitaani wafike kwenye ofisi zao na kupata leseni hiyo.