Klabu ya Tallis yatoa siri ya ubingwa kuogelea

By Shufaa Lyimo , Nipashe
Published at 09:34 AM Apr 23 2024

Waogeleaji wa Klabu ya Tallis.
Picha: Maktaba
Waogeleaji wa Klabu ya Tallis.

WAOGELEAJI wa Klabu ya Tallis wametoa siri ya mafanikio baada ya kuibuka mabingwa kwenye mashindano ya Klabu ya Taifa ya Kuogelea yaliyomalizika juzi, Jumapili kwenye Bwawa la Kuogelea la Shule ya Kimataifa Tanganyika (IST), iliyopo Masaki, Dar es Salaam.

Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti baada ya ushindi huo, walisema siri kubwa ya mafanikio hayo ni kufuata vema maelekezo waliyopewa na Kocha wao Mkuu, Alexander Mwaipasi, pamoja na kufanya juhudi mazoezini. 

Crissa Dillip mmoja wa wachezaji wa klabu hiyo, alisema mashindano yalikuwa na ushindani mkubwa, lakini alipambana mpaka kufanikiwa kuipa ushindi klabu yake huku akiahidi kufika mbali zaidi kupitia mchezo huo. 

Alisema anashukuru ameweza kuvunja rekodi kwa kuhakikisha anapunguza muda na kuwataka wazazi kuwaruhusu watoto wao wajifunze mchezo wa kuogelea.

Naye Raya Angemi, alisema siri ya ushindi huo ni kutokana na  mazoezi waliyokuwa wanayafanya mara kwa mara kwani bila hivyo wasingefika walipo sasa.

"Ninashukuru kwa matokeo haya kwani tumefanya juhudi kubwa mpaka tumefanikiwa, malengo yangu ni kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya kimataifa," alisema Angemi. 

Meneja wa Klabu ya Tallis, Hadija Shebe: "Tulijipanga kuhakikisha tunapata ubingwa, hii ni mara sita mfululizo Japokuwa kulikuwa na upinzani tumeweza kutetea kombe letu."

Wakati huo huo Mkurugenzi wa Ufundi wa Chama cha Mchezo wa Kuogelea Tanzania (TSA),  Amina Mfaume, alisema waogeleaji hao wameonyesha ushindani mkubwa, kwani wengi wao wamefanikiwa kupunguza muda wao. 

Klabu ya Tallis imebeba ubingwa huo baada ya kukusanya pointi 385 ikifuatiwa na Klabu ya Dar Swimming yenye pointi 330.