Benchikha aweka wazi wakusajiliwa

By Saada Akida , Nipashe
Published at 09:15 AM Apr 08 2024
 Kocha Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha.
Picha: Simba SC
Kocha Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha.

BAADA ya kushuhudia timu yake ikitolewa kwenye hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu wa tano sasa, Kocha Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha, ameweka wazi kuna kazi ya ziada inabidi kufanyika, ikiwamo kusajili washambuliaji wenye uwezo mkubwa wa kutumia nafasi zinazopatikana.

Simba jana ilirejea nchini ikitokea Misri ambapo ilikubali kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Al Ahly, hivyo kutupwa nje kwa jumla ya mabao 3-0 kutokana na mechi ya awali nyumbali katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kufungwa bao 1-0.

Akizungumza na Nipashe jana baada ya kurejea nchini,  Benchikha alisema pia kupoteza mchezo wa kwanza nyumbani dhidi ya Al Ahly uliongeza ugumu kwenye mechi ya marudiano, lakini akidai kuna mambo wamejifunza na kuahidi kuyafanyia kazi kwa msimu ujao ili kuwa bora zaidi.

Benchikha alisema Al Ahly ni timu bora na ina wachezaji wenye uzoefu ambao wanaweza kubadili mchezo muda wowote na hilo ndilo lililowagharimu, ikiwamo kupoteza nafasi nyingi kwenye mechi ya kwanza nchini.

“Lakini hatukuzitumia nafasi na wenzetu walipata moja pekee na waliitumia hiyo hiyo, ninaimani msimu ujao tukishiriki michuano hii tutakuwa bora zaidi kwa kuwa tutakuwa tumejifunza mengi, ikiwamo kuongeza baadhi ya wachezaji wenye uzoefu ambao wataongeza nguvu kwa waliopo hususan washambuliaji.

"Nafikiri kupoteza mechi ya kwanza nyumbani ndipo tulipoongeza ugumu wa mechi ya marudiano, Al Ahly ni timu bora na ina wachezaji wenye uzoefu wa michuano hii. Tumejifunza na naamini tutakuwa bora katika michuano hii mwakani kama tukipata nafasi ya kushiriki,” alisema  Benchikha.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally, alisema hawajilaumu kwa kutolewa na Al Ahly katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika bali wamejifunza ili wakati mwingine washiriki wakiwa bora zaidi.

Alisema hawana ubovu huo unaotwajwa kwa sababu timu imeweza kufikia hatua ya robo fainali ambayo imezoeleka na sasa wanaenda kutengeneza utamaduni wa kucheza nusu fainali.

“Hakuna ubovu huo unaoimbwa, sasa tunaenda kutengeneza timu, nusu fainali si rahisi, lazima tupambane na kuwekeza kwa kupata watu wa kutupeleka huko.

"Tupo katika mchakato huu wa kuwekeza kwa kuleta watu wenye uzoefu wa kucheza nusu fainali kuja kuungana na waliopo sasa kupigania timu kufika hatua hiyo ambayo Wanasimba wanaiota,” alisema Ahmed.

Aliongeza kuwa wanafanya kazi kubwa kurekebisha makosa yaliyojitokeza kwenye michezo yote miwili na kujiandaa kwa msimu ujao. 

“Al Ahly, Mabingwa watetezi wa michuano hii, ndio timu ya Karne ya Afrika na pia kinara wa kuchukua mara nyingi taji hili kwa hiyo kutolewa nao si jambo la kusema tutakaa na kuanza kujilaumu,” alisema Meneja huyo.

Kwa upande wa beki wa Kimataifa wa Simba, Che Fondoh Malone, alisema ameumia sana kwa timu yake kuondolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini hawana jinsi wanasahau yote na sasa kujiandaa na michezo iliyopo mbele yao.

Alisema wanatakiwa kujipanga kwa ajili ya mashindano mengi kuhakikisha wanafanya vizuri na kuipambania heshima ya nembo ya Simba katika michuano mingine ikiwamo Ligi Kuu na Kombe la CRBD Bank Federation .

Che Malone alisema hakuna mchezaji ambaye atafurahishwa na matokeo waliyoyapata nchini Misri na anaimani ni mpira na sasa wanajipanga kwa michezo ijayo.

“Tunasahau mchezo uliopita na sasa tunaangalia kilichopo mbele yetu, imeuma lakini hatuwezi kuendelea kuwaza kilichopata na tunahitaji kufanya vizuri kwenye michezo iliyopo mbele yetu na kusonga mbele,” alisema beki huyo.

Kikosi cha Simba kimeondoka jana kuelekea Kigoma tayari kwa mchezo wa hatua ya 16-bora ya Kombe la CRDB Federation dhidi ya Mashujaa FC utakaopigwa kesho katika Uwanja wa Lake Tanganyika.