Vifaa vitano vipya Simba hivi hapa

By Saada Akida , Nipashe
Published at 08:55 AM Apr 15 2024
Mshambuliaji  Foday Trawelly kutoka Brikama United.
Picha: Africa foot
Mshambuliaji Foday Trawelly kutoka Brikama United.

WAKATI Simba ikijiandaa kwa Derby ya Kariakoo, dhidi ya Yanga Aprili 20, mwaka huu, uongozi wa klabu hiyo umeanza kuingia chimbo na kusaka nyota wa kuwasajili huku majina ya baadhi ya majina ya wachezaji watano ambao tayari mazungumzo yameanza, yakifahamika.

Simba imekuwa katika presha kubwa kutokana na timu yao kutofanya vizuri baada ya kutupwa nje kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na kisha kutolewa katika michuano ya CRDB Federation Cup, maarufu Kombe la FA, huku ikianza kuwa na mwendelezo mbaya Ligi Kuu Bara.  

Nyota wanaotajwa mambo kuwa mazuri katika mazungumzo yao na Simba ni Chickna Diekite anacheza winga wa kushoto katika Klabu ya Real Bamako ya nchini Mali, Derrick Fordjour kutoka Klabu ya Medeama SC ya Ghana, mshambuliaji  Foday Trawelly kutoka Brikama United na Rodger Torach kutoka klabu ya Vipers ya Uganda anacheza beki.

Kadhalika Simba inadaiwa imepeleka ofa kwa uongozi wa Singida Fountain Gate FC kuhitaji saini ya Nickson Kibabage ambaye anacheza Yanga kwa mkopo ambao unaisha mwishoni mwa msimu huu.

Taarifa kutoka ndani ya Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, tayari majina hayo yapo mezani kwa ajili ya kujadiliwa kutokana na nafasi ambazo zimependekezwa na Kocha Abdelhak Benchikha kuboreshwa.

Imeelezwa kuna baadhi ya wachezaji ambao kocha anawahitaji kwa kutaja nafasi hivyo, kazi kubwa imefanywa na skauti kuangalia aina ya wachezaji na kwamba wapo wengi wanaotarajiwa kutemwa mikataba yao ikimalizika.

“Kuna wachezaji ambao msimu ujao hawatakuwa sehemu ya kikosi akiwamo Saido Ntibazonkiza mkataba wake unafika ukingoni, Aubin Kramo huenda akaenda kwa mkopo Zesco ya Zambia na Henock Inonga yupo sokoni muda wowote anaweza kupigwa bei,” kilidokeza chanzo hicho.

Aliongeza kuwa kabla ya msimu huo kumalizika Benchikha atakutana na Mwekezaji Mohamed 'Mo' Dewji kwa ajili ya kufanya tathimini ikiwamo wachezaji watakaochwa na wakuongezwa msimu ujao.

Kwa mujibu wa mwekezaji huyo, atakutana na Benchikha kujadili na kufanya tathimini ya timu yao na kuangalia nani wa kumtema na wakumuongeza kulingana na mapendekezo yake.

Katika hatua nyingine Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola, amesema wana kazi kubwa hususan katika safu ya ushambuliaji ambayo imekuwa ikishindwa kuzitumia nafasi wanazotengeneza.

Alisema wameumizwa kupoteza pointi mbili mbele ya Ihefu FC,  kwa sababu wamecheza mpira mzuri na kumiliki huku wakitengeneza nafasi, lakini wameshindwa kuzitumia na kupoteza alama mbili.

“Tatizo letu liko pale pale, kushindwa kutumia nafasi, ukiangalia Freddy (Michael) angekuwa makini tungepata matokeo, tunaenda kujiuliza na kufanyia kazi makosa hayo tukijiandaa na mchezo wetu dhidi ya Yanga.

Bado tupo katika mbio za ubingwa hatujakata tamaa na tunaenda kujipanga kwa ajili ya kusaka pointi tatu katika mchezo wetu wa Derby, ninaimani tutafanya vizuri,” alisema Matola.

Mechi ya watani wa jadi inatarajia kuchezwa Jumamosi wiki hii katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam huku Yanga ikiwa wenyeji wa mchezo huo.