Azam Complex kuwekwa viti kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:51 AM Jun 21 2024
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Thabit Zacharia.
Picha: Mtandao
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Thabit Zacharia.

UWANJA wa Azam Complex, uliopo Chamazi, Dar es Salaam, unatarajiwa kuwekwa viti wiki hii kwa ajili ya kuuwezesha kutumika kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Thabit Zacharia, amesema pamoja na mambo mengine, ukarabati huo unalenga zaidi kuuwezesha uwanja ukidhi mahitaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Africa (CAF) ili kuruhusiwa kuchezewa michuano hiyo ya kimataifa.

Azam msimu huu itashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya kushika nafasi ya pili kwenye msimamo Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliomalizika hivi karibuni.

"Tayari tumeshaleta viti, ndani ya wiki hii vitaanza kufungwa uwanja mzima. Kwa maana hiyo uwanja upo kwenye maboresho na Ligi ya Mabingwa msimu ujao itapigwa hapo," alisema Thabit, maarufu mama Zaka Zakazi.

Alisema hayo yote ni kuhakikisha klabu inakuwa na miundombinu ya uhakika na viti bora kama ambavyo wamekuwa hivyo miaka yote.

Awali uwanja huo ulikuwa unatumika kwenye michuano ya kimataifa, lakini baadaye CAF ilikuja na muongozo mpya, ikitaka viwanja vyote vitakavyochezewa michezo ya kimataifa kuwa na viti vya kukalia mashabiki, kitu ambacho kilikosekana katika uwanja huo ambao sehemu za kukaa mashabiki zimetengenezwa kwa mtindo wa mabenchi.

Hali hiyo ilipeleka CAF kuufungia uwanja huo, na athari zilionekana kwa klabu za Simba na Yanga msimu uliopita zilipokuwa zinahangaika kupata sehemu ya kucheza mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya Uwanja wa Benjamin Mkapa kufungwa kutokana na matengenezo.

Busara ya serikali ndiyo iliyotatua tatizo hilo na kwa kuziruhusu kucheza michezo ya kimataifa tu kwenye uwanja wa Mkapa.