Biashara United, Mbeya Kwanza vita muhimu leo

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 06:45 AM May 26 2024
Mpira golini.
Picha: Mtandaoni
Mpira golini.

TIMU ya Mbeya Kwanza inatarajia kuivaa Biashara United leo katika mechi ya marudiano ya kusaka tiketi ya kurejea Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani, Mtwara.

Katika mechi ya mkondo wa kwanza, Mbeya Kwanza ilipata kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Biashara United, mchezo uliopigwa Mei 19, mwaka huu kwenye Uwanja wa Karume Musoma mkoani, Mara.

Ili kuvuka hatua hiyo, Mbeya Kwanza itakazimika kushinda kuanzia mabao 3-0 na kuendelea ili kuingia hatua inayofuata kwa ajili ya kuzisubiri timu zitakazomaliza nafasi ya 13 na 14 kutoka kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mshindi kati ya timu hizo mbili, Biashara United au Mbeya Kwanza ambazo zilishuka daraja kutoka Ligi Kuu msimu mmoja wa 2021/22, anaweza kurejea tena pale atakapopata ushindi dhidi ya timu moja kati ya mbili zitakazotoana katika mechi za 'play off.'

Timu hizo zimelazikika kucheza mchujo, baada ya kumaliza nafasi ya tatu na ya nne katika Ligi ya Championship msimu uliomalizika kwa KenGold kutangazwa mabingwa wapya.

Mbeya Kwanza ilimaliza nafasi ya tatu ikiwa na pointi zake 65, Biashara United ikiwa na nne, ilikusanya pointi 62, huku ikiziacha KenGold na Pamba zikipanda Ligi Kuu moja kwa moja.

Msimu uliopita, Mashujaa FC ya Kigoma ilipanda Ligi Kuu kwa kushinda mechi yake ya 'play off' dhidi ya Mbeya City ambayo ililazimika kucheza mchezo huo, baada ya kufungwa na KMC katika michezo miwili ya mchujo, nyumbani na ugenini.

Ligi Kuu Tanzania Bara inatarajiwa kumalizika keshokutwa, hivyo timu zitakazoshuka daraja moja kwa moja na zile zinazosubiriwa kucheza mechi za mtoano zitajulikana baada ya pazi la ligi hiyo kufungwa rasmi.

Tayari Yanga imeshatangazwa kuwa mabingwa wapya wa msimu huu wa 2023/2024.