CECAFA Chalenji yapigwa kalenda

By Hawa Abdallah , Nipashe
Published at 07:35 AM Apr 22 2024
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), Hussein Ahmada Vuai.
Picha: Maktaba
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), Hussein Ahmada Vuai.

MASHINDANO ya CECAFA Senior Chalenji ambayo kwa mwaka huu yatafanyika hapa Visiwani Zanzibar, yamesogezwa mbele hadi Julai 6, badala ya Juni 29, tarehe iliyopangwa hapo awali.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), Hussein Ahmada Vuai, akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana, alisema kusogezwa mbele kwa mashindano hayo kumetokana na sababu ambazo zipo nje ya uwezo wao, ikiwamo ombi la wadhamini ambao wameomba kufanyika mwezi huo.

Alisema matarajio yao katika mashindano hayo ni kuwapo kwa  ushindani mkali kwa nchi shiriki, ambapo sasa yataanza Julai 6 hadi 21, mwaka huu.

Vuai alisema maandalizi yanakwenda vizuri na tayari timu ya CECAFA ambayo walikuwa na ukaguzi wa miundombinu kwa ujumla wake kwa ajili ya mashindano ya shule kwa vijana walipata nafasi hiyo ya kukagua miundombinu yote ya Zanzibar kwa hatua ya awali.

Aidha, alisema timu hiyo ya ukaguzi, inatarajiwa kuja tena kufanya ukaguzi huo kutokana na taratibu zao, ingawa wameridhishwa na hali ya  miundombinu ya hapa nchini.

“Wazanzibari wajiandae mashindano yapo na tunatarajia ukaguzi wa awamu ya pili ambao ndio wa mwisho utakaofanyika ndani ya mwezi ujao, lakini tunaamini kila kitu kinakwenda vizuri,” alisema.

Hata hivyo, alisema mpaka sasa wamekuwa na ushirikiano mzuri na wanajiandaa vema kuhakikisha mashindano hayo yanafanikiwa.