Chama, Aziz Ki wawindwa Azam

By Saada Akida , Nipashe
Published at 09:27 AM Apr 23 2024
news
Pi Maktaba
Kiungo mnyumbulifu, Clatous Chama,akisalimiana na mchezaji wa Yanga SC, Stephane Aziz Ki .

KOCHA wa Azam FC, Youssouph Dabo, ametaja wachezaji watano kutoka Simba na Yanga, ambao amewapendekeza kwa uongozi wa timu hiyo ili kupata huduma zao kwa ajili ya msimu ujao wa mashindano.

Kutoka Simba, Dabo anahitaji huduma ya kiungo mnyumbulifu, Clatous Chama, ambaye  mkataba wake upo ukingoni na Kibu Denis kwa ajili ya kutaka kuimarisha kikosi chake kwa msimu wa 2024/25.

Kwa upande wa Yanga wachezaji Dabo anaotaka kufanya nao kazi ni kipa Djigui Diarra, Stephane Aziz Ki ambaye naye mkataba wake unatamatika mwishoni mwa msimu huu na Clement Mzize ambaye majuma yaliyopita aliongeza mkataba wa miaka miwili.

Akizungumza na Nipashe jana, Dabo alisema amewafuatilia wachezaji hao na kujiridhisha wako vizuri na tayari majina amependekeza kwa uongozi wao kwenye mipango yao ya usajili kwa ajili ya kuboresha timu kuelekea msimu ujao wa mashindano.

“Si Mzize pekee ndio tunataka bali kuna Diarra na Aziz Ki pale Yanga, Simba tunahitaji wachezaji wawili Chama na Kibu. Ni wachezaji wazuri, mambo yakienda vizuri ninaimani tutapata huduma za nyota hao,” alisema Dabo.

Tayari Azam ilishaweka wazi kuwa imeulizia uwezekano wa kuipata huduma ya Mzize, ikisema inataka kupata mshambuliaji asilia wa nafasi hiyo kutokana na kuwa katika mvutano wa kuvunja mkataba straika wao, Prince Dube.

Dube tayari ameondoka Azam FC akishinikiza kuvunja mkataba na klabu hiyo huku akiweka wazi hana mapenzi tena na timu hiyo anataka kwenda kujaribu bahati kwingineko.

Mshambuliaji huyo raia wa Zimbabwe, ambaye  amekuwa akihusishwa na Yanga, alifikisha kesi yake ya kimkataba na Azam FC, kwa Shirikisho la Soka nchini (TFF), lakini waajiri wake hao walishinda. 

Kuhusu suala la ubingwa msimu huu, Dabo amesema kulingana na muelekeo wa timu yake wako katika reli ya kuwania taji hilo kutokana na tofauti ya pointi nne kati ya aliyekuwa juu yao, Yanga.

Katika msimamo Azam FC inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 54 ilizozikusanya kutokana na michezo 24 na Yanga wanaongoza ligi kwa pointi 58, kwa michezo 22 huku Simba ikishika nafasi ya tatu kwa alama 46 ilizozipata kutokana na mechi 21 ilizocheza hadi sasa msimu huu.