Dabi 6 zisizosahaulika

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 06:17 AM Apr 20 2024
Kibu Denis, akipiga mpira kwa kichwa kuelekea katika lango la Yanga katika mchezo uliozikutanisha timu hizo mbili ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa goli 5-1.
Picha: Maktaba
Kibu Denis, akipiga mpira kwa kichwa kuelekea katika lango la Yanga katika mchezo uliozikutanisha timu hizo mbili ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa goli 5-1.

MASHABIKI wa soka ndani na nje ya Tanzania wanatarajia kusimama kwa dakika 90 ili kushuhudia mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Ni mchezo ambao unaongeza idadi ya mechi za watani wa jadi, yenye majina mengi, wengine wakiita Dabi ya Kariakoo, lakini kama kawaida, huingizwa katika vitabu vya kumbukumbu za soka na kusomwa na vizazi hadi vizazi pale watakapohitaji kupekua rekodi zake.

Rasmi rekodi za timu hizi zilianza kuwekwa mwaka 1968, ambapo pamoja na mechi nyingi kuchezwa, lakini kuna michezo kadhaa imebaki katika kumbukumbu hadi leo kutokana na matokeo yake ya kushangaza, vipigo vikubwa na kuweka rekodi ambazo hazijavunjwa.

Hizi ni baadhi ya mechi ambazo hadi leo zimebaki ni simulizi katika mechi za dabi. 

1. Yanga 5-0 Simba (1968)

Mechi hii imeingia katika rekodi ya kuwa ni ya kwanza timu hizo kufungana mabao mengi katika mechi za dabi. Hii ilikuwa ni Juni Mosi, mwaka 1968. Yanga ikiiadhibu Simba mabao 5-0, ambayo yalifungwa na Maulidi Dilunga (mawili), Kitwana Manara (mawili) na Salehe Zimbwe alifunga bao moja. 

2. Simba 6-0 Yanga (1977) 

Simba ililipa kisasi cha kufungwa mabao 5-0 miaka tisa baadaye, ilipoikandika Yanga magoli 6-0, mechi ambayo hadi leo inashika rekodi ya timu kufungwa mabao mengi zaidi katika dabi.

Ni mechi ambayo pia imeweka rekodi ambao haijavunjwa kwa mshambuliaji wake, Abdallah Kibadeni 'King' kufunga hat-trick'.

Mechi ilichezwa Julai 19, mwaka 1977, na mbali na King Kibadeni, mabao mengine mawili yalifungwa na Jumanne Hassan 'Masimanti' na beki, Selemani Sanga wa Yanga akijifunga mwenyewe. 

3. Simba 4-4 Yanga (1996) 

Mechi hii inabaki katika vitabu vya kumbukumbu kuwa ndiyo sare iliyozaa mabao mengi zaidi kwenye mchezo wa dabi.

Mechi ilichezwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini, Arusha, mabao ya Yanga yakifungwa na Edibily Lunyamila, Mustapha Hozza (akijifunga), Said Mwamba 'Kizota' na Sanifu Lazaro, huku ya Simba yakipachikwa na Thomas Kipese, Ahmed Mwinyimkuu na Dua Said akipiga mawili. 

4. Simba 5-0 Yanga (2011/12) 

Ni moja kati ya mechi za kukumbukwa za watani wa jadi, ikichezwa Mei 6, mwaka 2012, Simba ilipata matokeo hayo kupitia mabao yaliyowekwa kimiani na Emmanuel Okwi, aliyefunga mawili, Felix Sunzu, Patrick Mafisango (marehemu) na Juma Kaseja, wote wakifunga magoli hayo kwa  penalti. 

5. Simba 3-3 Yanga (2013/14) 

Ilikuwa ni moja kati ya dabi za kushangaza ambapo hadi mapumziko Yanga ilikuwa ikiongoza mabao 3-0, lakini Simba ikarudisha magoli yote kipindi cha pili.

Dabi hiyo ilichezwa Oktoba 20, mwaka 2013, Yanga ikitangulia kwa mabao ya Mrisho Ngassa na Hamisi Kiiza wakati  Simba ilisawazisha kupitia Betram Mombeki, Joseph Owino na Gilbert Kaze. 

6. Yanga 5-1 Simba (2023/24) 

Hii ni dabi ya mzunguko wa kwanza msimu huu, ambapo Yanga ilitoa kipigo kikubwa cha mabao 5-1, mechi iliyochezwa Novemba 5, mwaka jana.

Yalikuwa ni mabao ya Kennedy Musonda, Maxi Nzengeli (mawili), Stephane Aziz Ki na Pacome Zouzoua.