KOCHA Mkuu wa Azam FC, Youssouph Dabo, amekiri kuwapo kwa ugumu wa Ligi Kuu Tanzania Bara hususani mzunguko wa pili ambao kila timu inahitaji ushindi ili kufikia malengo yao.
Dabo aliliambia gazeti hili kwa upande wao wanahitaji alama muhimu kwa kila mechi watakayocheza kwa lengo la kujihakikishia wanamaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo ili kupata tiketi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kocha huyo alisema mikakati yake ni kuona timu yake inafikia malengo ambayo waliyaweka tangu mwanzoni mwa msimu na watapambana ili kufikia ndoto zao.
“Sio rahisi kushinda mechi zote, tunauwezo wa kumfunga kila mpinzani anayekuja mbele yetu, lakini kuna wakati mwingine tukubali hatuwezi kushinda kwa kila mechi. Tunahitaji umakini zaidi katika mechi zetu zijazo kwa sababu hakuna mchezo utakaouwa rahisi,” alisema kocha huyo.
Aliongeza anaandaa kikosi imara kwa kuwapa mbinu za kiufundi mbalimbali na kuwaweka sawa kisaikolojia kutokana na ushindani uliopo kwenye hatua hii ya lala salama.
Dabo alisema pia malengo yake mengine ni kufanya vyema katika mchezo wao wa hatua ya robo fainali ya mashindano ya Kombe la Shirikisho la CRBD Bank dhidi ya Namungo utakaochezwa kati ya Mei 2 na 4, mwaka huu.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED