Diarra, Matampi wafungana

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:15 AM May 16 2024
Golikipa wa Yanga, Djigui Diarra (kushoto) na  wa Coastal Union, Ley Matampi.
Picha: Mtandaoni
Golikipa wa Yanga, Djigui Diarra (kushoto) na wa Coastal Union, Ley Matampi.

KIPA raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wa Coastal Union, Ley Matampi, amefikisha idadi ya mechi 13 alizokaa langoni bila kuruhusu bao katika mechi za Ligi Kuu inayoelekea ukingoni, akimfikia Djigui Diarra wa Yanga.

Matampi, ambaye tetesi zinasema anawaniwa na Simba, amefikisha 'clean sheets' 13, baada ya kutoruhusu wavu wake kuguswa katika mechi ya juzi walipocheza dhidi ya Geita Gold FC kwenye Uwanja wa Nyankumbu, Geita.

Awali, Diarra, raia wa Mali, alikuwa anaongoza, huku mwenzake akiwa na 'clean sheets' 12, lakini alishindwa kuongeza baada ya kuruhusu bao katika mechi ya Jumatatu iliyopita, ikichezwa, Uwanja wa Manungu Complex, Turiani, Morogoro, timu yake iliposhinda mabao 3-1.

Matampi, aliyesajiliwa msimu huu akitokea klabu ya Renaissance ya DR Congo,  amekuwa katika kiwango cha hali ya juu akicheza kwa mara ya kwanza, Ligi Kuu Tanzania Bara kiasi cha kuivutia Simba.

"Tunamhitaji kipa huyu, ni mzuri sana, kama anacheza katika klabu ya kawaida kama Coastal Union, tukimpata sisi, na tutakuwa tumefanya usajili wa mabeki bora, atakuwa kwenye kiwango cha juu zaidi kuliko hata hapa alivyo," kilisema chanzo chetu.

Baada ya Yanga kutwaa ubingwa, hivi sasa vita iliyobakia ni ya kumaliza msimu katika nafasi ya pili huku hekaheka nyingine ikiwa ni kupambana kusalia kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.

Stephane Aziz Ki wa Yanga na Feisal Salum na Azam, kila mmoja akiwa na mabao 15, wao wako katika vita ya kuwania kiatu cha dhahabu huku mchezaji anayeongoza kwa kutoa pasi nyingi za mabao akiwa ni Aziz Ki akifuatiwa na Kipre Junior wa Azam FC.