Mabingwa Mtoko wa Kibingwa watua, wamtaja Aziz Ki, Chama

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:25 AM Apr 20 2024
Balozi wa Kampuni ya Betika, Baraka Mpenja (mwenye suruali ya kaki), akiwa na baadhi ya washindi wa Mtoko wa Kibingwa baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam tayari kuishuhudia dabi ya Simba na Yanga
Picha: Mpigapicha Wetu
Balozi wa Kampuni ya Betika, Baraka Mpenja (mwenye suruali ya kaki), akiwa na baadhi ya washindi wa Mtoko wa Kibingwa baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam tayari kuishuhudia dabi ya Simba na Yanga

WAKATI mashabiki wakihesabu saa chache ili kufanyika mechi ya marudiano ya watani wa jadi, Simba na Yanga katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu itakayochezwa leo, mabingwa wa Mtoko wa Kibingwa wamewasili Dar es Salaam tayari kuishuhudia dabi hiyo.

Mabingwa hao ambao ni washindi wa kampeni ya Mtoko wa Kibingwa iliyotoa fursa kwa mashabiki 56 kuishuhudia dabi hiyo kwa hadhi ya VIP kwa gharama za Betika, wamewasili jijini na kuwataja nyota wa timu hizo, Stephanie Aziz Ki wa Yanga na Clatous Chama wa Simba  ndio wanawatarajia kuamua mechi hiyo.

Wengi wao kutoka nje ya Dar es Salaam wamesema, hii ndiyo mara yao ya kwanza kuishuhudia dabi hiyo 'laivu', na hata kusafiri kwa ndege.

"Betika waliponipigia simu nilikuwa shambani, sikuamini, nilihisi ni utani, ila nikasema ngoja niende nao hadi mwisho nione itajavyokuwa," alisema Uria Mtalika wa Kaliua mkoani, Tabora.

Shabiki huyo kindaki ndaki wa Yanga alisema, Jumatano iliyopita alitoka Kaliua hadi Tabora mjini kama alivyoelekezwa na mwakilishi wa Betika.

"Niliendelea kuwasiliana nao, lakini sikuwa naamini hadi nilipopanda ndege na leo (jana) nipo Dar nikisubiri kuishuhudia dabi," alisema Mtalika huku akiitabiria timu yake ushindi wa mabao 2-0.

Mshindi mwingine, Kimara Mapunda kutoka Sumbawanga aliliambia gazeti hili mechi ya leo roho yake ipo kwa Simba.

"Nawashukuru Betika kwa kuweka fursa ya Mtoko wa Kibingwa, nilicheza bila kukata tamaa hadi nimeshinda na kuja kutizama dabi, hii ni mara yangu ya kwanza kushuhudia dabi, kinachonivutia zaidi ni kuja kuwaona wachezaji wa Simba hasa Chama na Kibu Denis, nawakubali sana," alisema.

Naye shabiki wa Simba, Mussa John, wa Arusha alisema anaamini watalipa kisasi leo kwa kuichapa Yanga mabao matano huku Clinton Festo wa Kigoma alisema hana shaka na timu yake kupata matokeo, lakini Aziz Ki na Pacome anaamini wataiduwaza Simba.

Akizungumza mara baada ya kuwapokea mabingwa hao, Balozi wa kampeni hiyo msimu huu, Baraka Mpenja, alisema mashabiki wote wataishuhudia dabi kwa hadhi ya VIP.

"Hawa wa mikoani wataungana na mabingwa wetu wa Dar es Salaam ambao leo (jana) watalala kwenye hoteli ya nyota tano kabla ya kwenda uwanjani wakiongozwa na king'ora kushuhidia dabi hiyo wakiwa kwenye jukwaa la VIP," alisema Mpenja.

Mbali na mabingwa, Ofisa Habari wa Betika, Juvelinaus Rugambwa, alisema  kulikuwa na zawadi mbalimbali za wiki na mwezi kwenye kampeni hiyo.

"Kila wiki tulikuwa na washindi wa simu janja aina ya tecno na kila mwezi tulikuwa na washindi wawili wa iphone 15 ili kunogesha kampeni yetu hadi leo (jana) tumewapokea mabingwa wetu.

"Betika ni bandika bandua, hatuna mbambamba, baada ya dabi, mashabiki wetu wakae mkao wa kitu kingine bomba," alisema Rugambwa.