Pacome fiti 100% kuitumikia Yanga

By Saada Akida ,, Shufaa Lyimo , Nipashe
Published at 06:01 AM Apr 18 2024
news
Picha: Yanga SC
Kiungo Mshambuliaji wa Yanga, Pacome Zouzoua.

ZIKIWA siku mbili kabla ya mechi ya 'Derby' ya Kariakoo, Kiungo Mshambuliaji wa Yanga, Pacome Zouzoua, ameanza mazoezi ya ushindani na wachezaji wenzake baada ya kukaa nje ya uwanja kwa siku 29 akiuguza jeraha la nyama za paja.

Yanga itaikaribisha Simba kwenye Derby ya Kariakoo, keshokutwa, Jumamosi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, ikiwa ni mechi ya raundi ya pili ya Ligi Kuu Tanzania Bara. 

Nyota huyo raia wa Ivory Coast, aliumia katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC, uliochezwa Mei 17, mwaka huu, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam, Yanga wakikubali kichapo cha mabao 2-1. 

Akizungumza na Nipashe jana, Daktari wa Yanga, Moses Etutu, alisema Pacome amerejea kwenye uwanja wa mazoezi na  anaendelea vizuri katika mazoezi ya ushindani na wenzake.

Alisema awali nyota huyo alikuwa na program maalum ya mazoezi yake binafsi kwa siku alizopewa lakini kwa sasa amerejea uwanjani na kuendelea na majukumu yake ndani ya timu hiyo kama kawaida.

"Pacome tayari ameanza mazoezi na wenzake, kuhusu kumtumia katika mchezo ijao hiyo ni kazi ya benchi la ufundi, kumpa nafasi au kuendelea kumsubiri na kumpa dakika chache za kucheza kwa ajili ya kuwa fiti zaidi,” alisema Daktari huyo. 

Ofisa habari wa Yanga, Ali Kamwe, alisema nyota huyo ameanza kufanya mazoezi lakini hakuna ulazima wa kocha wa timu hiyo Miguel Gamondi, kulazimika kumtumia kwa mechi ya Derby ya Kariakoo. 

“Wachezaji wetu ambao walikuwa majeruhi wameanza kupona na kurudi uwanjani, akiwamo Pacome, lakini hatuwezi kulazimisha mchezaji aliyetoka kwenye majeraha kumpanga kucheza katika mechi kubwa na ngumu kama hii dhidi ya Simba,” alisema Kamwe.

Kiungo huyo baada ya kuumia, Yanga imecheza michezo minne, miwili ya Ligi ya Mabingwa wakitolewa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kwa penalti 3-2 baada ya kusuluhu katika michezo yote miwili ya nyumbani na ugenini.

Baada ya hapo Yanga ilicheza mchezo wa hatua ya 16-bora ya Kombe la Shirikisho, FA Cup dhidi ya Dodoma Jiji wakishinda mabao 2-0 na kutinga hatua ya nusu fainali.

Pia, ilicheza mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Singida Fountain Gate na kuibuka na ushindi wa mabao 3-0, mchezo uliochezwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Katika hatua nyingine, uongozi wa Klabu ya Azam FC, umethibitisha kupeleka ofa Klabu ya Yanga ukionyesha nia ya kumtaka mshambuliaji wao, Clement Mzize.

Akithibitisha taarifa hiyo jana, Msemaji wa timu ya Azam FC, Thabit Zakaria 'Zaka za Kazi', alisema wamelazimika kupeleka ofa hiyo baada ya kuridhishwa na kiwango cha mshambuliaji huyo, huku wakieleza kwa sasa hawana mshambuliaji asilia katika timu yao. 

"Ni kweli tumepeleka ofa Yanga ya kumhitaji Mzize isipokuwa mpaka sasa bado hatujajibiwa endapo kama tutakubaliwa tutakaa meza moja na kufanya biashara kwa kuwa Yanga tulifanya nao biashara muda mrefu wakati tunamhitaji Mrisho Ngassa na iliwezekana," alisema Zaka za Kazi.

Alisema wameamua kumtafuta huduma ya Mzize kwa ajili ya kupanga mikakati kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ambapo usajili utaanza mapema mwezi Juni mwaka huu. 

Aidha, alisema hawamlazimishi aliyekuwa mshambuliaji wao, Prince Dube, kuichezea timu hiyo na badala yake anapaswa kufuata taratibu za mkataba ili wamruhusu aendelee na maisha yake. 

"Kuna ofa ambazo zilitumwa na Klabu ya Simba pamoja na Al Hilal ya Sudan, zikionyesha nia ya kumhitaji baada ya muda mfupi tutatoa taarifa ya hizo ofa ili Watanzania pamoja na mashabiki wetu wafahamu kinachoendelea," alisema.