Simba kufyeka tena wachezaji

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 12:36 PM Jan 24 2024
Kocha Mkuu Abdelhak Benchikha.
Na Mtandao
Kocha Mkuu Abdelhak Benchikha.

KLABU ya Simba imesema haijamaliza kuondoa wachezaji walioshuka viwango, au wote wasiojituma kwenye kikosi hicho na kutoa angalizo kuwa yeyote asiyefanya hivyo ataachwa mwishoni mwa msimu hata kama alisajiliwa kipindi cha dirisha dogo.


Mwenyekiti wa Bodi ya Klabu hiyo, Salim Abdallah 'Try Again', amesema zoezi la kufyeka wachezaji wote wavivu, walioshuka viwango na wasiojituma bado linaendelea na linafanywa na Kocha Mkuu Abdelhak Benchikha kwa kushirikiana na viongozi, hivyo kuwataka wachezaji wote waliopo sasa wafanye kazi ya kuipambania Simba na si vinginevyo.

"Dirisha kubwa linakuja, nasisitiza kusema tena huu tena si mjadala, hatutaangalia sura wala jina la mtu au wewe ni maarufu kiasi gani, au wapenzi wanakukubali kiasi gani, tunachotaka sisi ni kitu gani unatupa kwenye klabu yetu.

"Mchezaji umeajiriwa kazi yako ni kufanya kazi ya kuiletea ushindi Simba, ukishindwa tunakuondoa tunaweka mwingine kwa hiyo tutaendelea na panga hili kama kawaida, hivi sasa tunalinoa kwa ajili ya kufanya kazi mwishoni mwa msimu.

"Nitoe wito kwa wachezaji wote wafanye kazi ya kuisaidia klabu ya Simba, la sivyo 'thank you' itamhusu mwishoni mwa ligi," alisisitiza kiongozi huyo.

Tayari Simba imeshawatoa baadhi ya wachezaji na kuwapeleka wengine kwa mkopo mwishoni mwa dirisha dogo la usajili.

Wachezaji hao ni Jimmson Mwanuke na Nassor Kapama waliokwenda Mtibwa Sugar, Shaaban Chilunda akienda KMC, Jean Baleke aliyerejea TP Mazembe,  na Moses Phiri ambaye ameeleka Power Dynamos ya Zambia.

Timu hiyo imewasajili Babacar Sarr kama mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake na Klabu ya US Monastir ya Tunisia, Salehe Karabaka kutoka JKU ya Zanzibar, Omar Jobe kutoka Zhenis ya Kazakhstan, Freddy Michael Kouablan, akisajiliwa kutoka Green Eagles ya Zambia, na Ladack Chasambi kutoka Mtibwa Sugar.

Try Again alisema Benchikha ndiye aliyependekeza wachezaji waliosajiliwa na walioachwa, huku wengine wakiponea kwenye Kombe la Mapinduzi.

"Usajili huu ni mapendekezo ya mwalimu alitupa ripoti ya wachezaji wangapi tuwaache na wangapi tusajili na akatoa maelekezo ya maeneo ya kusajili na hata majina ya wachezaji akisema namtaka huyu.

"Kwa hiyo niseme tu kuwa usajili wetu umezingatia maekezo ya mwalimu na baadhi ya aliosema tuwaache wamekwenda kuponea Kombe la Mapinduzi, Zanzibar ambako baada ya kufanye vema akabadili msimamo wake na kuwabakisha kikosini," alisema.

Aliongeza kuwa watakaojituma kwenye nusu msimu huu wataendelea kuwapo, lakini watakaoonekana wanacheza chini ya kiwango watawaondoa hata kama walisajiliwa kipindi cha dirisha dogo.

"Awali, tuliwahi kusema kuwa mchezaji ambaye haonyeshi kiwango cha kujituma basi tutaachana naye, ndivyo itakavyokuwa na mwalimu wetu amebariki hilo, hata kama tulimsajili dirisha dogo ataondoka tu, msimu ujao tunataka kutengeneze kikosi cha wachezaji wenye uwezo mkubwa, wapambanaji na wenye nidhamu," alisema Try Again.