Simba waenda kujaribu bahati Muungano Cup

By Hawa Abdallah , Nipashe
Published at 09:31 AM Apr 23 2024
Nembo ya Shirikisho la Soka Tanzania na Shirikisho la Soka Zanzibar.
Picha: Maktaba
Nembo ya Shirikisho la Soka Tanzania na Shirikisho la Soka Zanzibar.

BAADA ya kutupwa nje kwenye robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika na kisha kuondoshwa Kombe la FA (CRDB Confederation Cup), huku ikiendelea kuvurunda kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, Klabu ya Simba leo inatarajia kuwasili Zanzibar tayari kwa ajili ya michuano ya Kombe la Muungano.

Michuano hiyo ambayo imeanzia moja kwa moja hatua ya nusu fainali, inaanza kesho kwa KVZ FC kuikaribisha Simba katika Uwanja wa New Amani Complex saa 2:15 usiku na kesho Jumatano itakuwa zamu ya Azam FC kuvaana na KMKM SC uwanjani hapo na muda huo huo, ikiwa ni fainali ya pili. Washindi wa mechi hizo watakutana fainali uwanjani hapo Aprili 27, mwaka huu.

Ni miaka 20 sasa imepita tangu michuano hiyo isimame kufanyika, ambapo msimu huu imerudi kwa kuanza na timu nne.

Akizungumza na gazeti hili jana Kocha Mkuu wa timu ya KVZ FC, Ali Mohmed Ameir, alisema  mipango yao ni kufika fainali katika mashindano hayo licha ya kukabiliwa na mchezo mgumu dhidi ya Simba ambayo ina uwezo na uzoefu mkubwa katika mashindano ya ndani na nje.

Alisema kikosi chake kimefanya mazoezi na tayari kimeshapata mechi moja katika michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), maarufu FA Cup, mchezo ambao aliangalia mapungufu yaliyojitokeza na kuyafanyia kazi mazoezini.

“Mchezo huu ni mgumu kwetu na tunawajua wapinzani wetu 'level'  yao katika soka, hivyo tutatumia mbimu ambayo itatufanya tupate ushindi,” alisema.

Akizungumzia maandalizi ya michuano hiyo, Katibu Mkuu wa ZFF, Hussein Ahmada Vuai, alisema kila kitu kimekamilika kuelekea mashindano hayo.

Alisema wanaendelea kushirikiana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ili kuhakikisha kila kitu kinakwenda kama kilivyopangwa.

Hata hivyo, aliwaomba Wazanzibar na Watanzania kwa Ujumla wote kwenda uwanjani katika kuyapa hamasa mashindano hayo.