BAADA ya kumkosa katika dirisha dogo la usajili lililofungwa Januari, mwaka huu, Klabu ya Simba imeacha tena mchakati wa kusaka huduma ya winga na kiungo mshambuliaji wa Ihefu, raia wa Togo, Marouf Tchakei.
Simba imepania kwa kiasi kikubwa kufumua kikosi chake na kutengeneza timu mpya yenye ushindani kwa ajili ya msimu ujao wa mashindano, inapiga hodi kwa kiungo huyo ambaye anacheza namba moja na Clatous Chama.
Habari kutoka ndani ya Simba zinasema huenda safari hii wanaweza nyota huyo kirahisi kutokana na kilichoelezwa pia nyota huyo yuko tayari kupata changamoto mpya lakini bado anabanwa na mkataba wake.
Chanzo chetu kingine kutoka Ihefu kimesema bado ana mkataba, hivyo kama Simba inamhitaji italazimika kufanya mazungumzo.
"Tulimhitaji dirisha dogo la usajili, lakini ilishindikana, klabu yake iliweka ngumu lakini mwenyewe alikuwa radhi kujiunga na timu yetu, akatuambia tusubiri msimu uishe atakuwa huru, sisi tunasimamia pale pale, lakini kama itakuwa vinginevyo basi tutaangalia itakavyokuwa lakini ni lazima tumng'oe, tumejidhihirisha ni mchezaji mzuri na atatusaidia sana, ameshaifahamu Ligi ya Tanzania na ameizoea," aliongeza mtoa taarifa wetu.
Chanzo hicho kiliongeza Ihefu ilimwongezea mkataba mpya Januari 24, mwaka huu baada ya uhamisho wake wa kujiunga na Wekundu wa Msimbazi kushindikana, hivyo waajiri wake wakaamua 'kumbana' ili asiondoke bure baada ya msimu huu kumalizika.
"Tunajua Simba wanamhitaji, na wamezungumza naye na yeye anahitaji kwenda huko, tulichofanya ni kumwongeza mkataba ili asiondoke bure, angalau na sisi tuambulie chochote," kilisema chanzo kutoka Ihefu.
Mchezaji huyo alijiunga na Singida Fountain Gate mwanzoni mwa msimu akitokea AS Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), kabla kuhamishwa na kupelekwa Ihefu, amekuwa katika kiwango cha hali ya juu na mwenye mchango kwa timu yake.
Nyota huyo amefunga mabao tisa msimu huu akiwa na timu zote mbili.
Wakati huo tetesi zinasema Simba ipo katika hatua za mwisho za kumalizana na mchambuzi wa video na viwango, Alexander Kerveillant kutoka Al Nassry ya Saudi Arabia kwa ajili ya kufanya kazi hiyo kuelekea msimu ujao wa mashindano.
Mchambuzi huyo raia wa Ufaransa anatajwa kurithi mikoba ya Culvin Mavunga ambaye amekuwa na kikosi hicho kwa muda mrefu sasa.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema hiki ni kipindi cha tetesi za usajili, na haizuiliki, lakini ukweli na kila kitu kitafahamika pale Ligi Kuu Tanzania Bara itakapomalizika.
"Siku zote huwezi kuzuia tetesi za usajili, ila sisi ni kweli tutasajili, tena usajili mkubwa tu, nani tutamsajili, ni kiasi cha kusubiri, Simba tumekuwa na utaratibu wetu wa kumtangaza kila anayekuja katika klabu yetu," alisema Ahmed.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED