Simba, Yanga rekodi kibao zatawala Dabi

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:41 AM Apr 22 2024
news
Picha: Mpigapicha Wetu
Wachezaji wa Simba na Yanga wakiwania mpira wa juu katika mechi ya 'Dabi' ya Kariakoo iliyopigwa juzi Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. Yanga ilishinda mabao 2-1.

MECHI ya watani wa jadi, iliyochezwa juzi, Uwanja wa Benjamin Mkapa, iliyomalizika kwa Yanga kuifunga Simba mabao 2-1, imeacha rekodi kadhaa ikiwamo mabao yote matatu kufungwa kwa mguu wa kushoto.

Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, mzunguko wa pili, mabao yote yalifungwa katika lango la Kusini na wachezaji wa kigeni watupu, huku Waivory Coast wawili, Joseph Guede wa Yanga na Freddy Michael, waliosajiliwa kipindi cha dirisha dogo, wakiweka rekodi ya kufunga mabao katika dabi zao za kwanza nchini.

Kiungo mshambuliaji wa Burkina Faso, Stephane Aziz Ki, aliingia kwenye rekodi ya kufunga mabao kwenye mechi zote mbili za msimu mmoja, akiifikia rekodi ya Amissi Tambwe aliyefanya hivyo msimu wa 2015/16.

Alifunga bao moja katika mechi ya mzunguko wa kwanza, Novemba 5, mwaka jana, kwenye uwanja huo huo, akiiongoza timu yake kushinda mabao 5-1.

Aziz Ki, pia ameendeleza rekodi yake nzuri ya kuifunga Simba, kwani hata msimu uliopita alifanya hivyo katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu katika mchezo wa dabi uliochezwa, Oktoba 23, 2022, na timu hizo kutoka sare ya bao 1-1, kabla ya Simba kuifunga Yanga mabao 2-0 katika mechi ya mzunguko wa pili iliyochezwa Aprili 16, 2023.

Baada ya yeye mwenyewe kufanyiwa madhambi na Hussein Kazi ndani ya eneo la hatari, Aziz Ki, raia wa Burkina Faso alifunga bao hilo kwa kutumia mguu wa kushoto dakika ya 19, kabla ya Guede kupachika la pili dakika ya 37,  alipopokea mpira mrefu uliopigwa kutoka katikati ya uwanja, akaumiliki peke yake mabeki wa Simba wakidhania kuwa ameotea, akamlamba chenga kipa Lakred kabla ya kuujaza wavuni.

Freddy alipachika bao la kufutia machozi kwa mguu wa kushoto dakika ya 73, akiitendea haki pasi ya Clatous Chama, akiwalambisha sakafu, Ibrahim Hamad 'Bacca' na Bakari Mwamnyeto, kabla ya kuukwamisha wavuni.

Mechi ya juzi imemfanya Aziz Ki, kuendelea kuongeza pengo la ufungaji katika Ligi Kuu baina yake na Feisal Salum wa Azam FC, akifikisha mabao 15, Freddy akifikisha manne, na Guede matatu.

Yanga imerudia rekodi yake iliyoiweka msimu wa 2015/16 kuifunga Simba mara mbili kwa msimu mmoja, ambapo ilikuwa mara ya mwisho kwa mechi za dabi timu moja kushinda mara hizo kwa msimu mmoja.

Mechi ya mzunguko wa kwanza ilishinda mabao 2-0, yaliyowekwa wavuni na Amissi Tambwe na Malimi Busungu na mzunguko wa pili ilishinda idadi hiyo hiyo ya mabao yaliyofungwa na Donald Ngoma na Tambwe.

Matokeo ya mechi hiyo yameifanya Yanga kuukaribia ubingwa kwa mara ya tatu mfululizo ikiwa imefikisha pointi 58, ikicheza mechi 22 na kusalia na michezo minane ikiendelea kujichimbia kileleni mwa msimamo Ligi Kuu, huku Simba iliyocheza michezo 21 mpaka sasa, ikisalia na pointi zake 46, ikiwa nafasi ya tatu, ikibakisha michezo tisa kabla ya kuhitimisha mechi zake za msimu huu.