Uhamiaji FC: Tutarudi Ligi Kuu na kasi mpya

By Hawa Abdallah , Nipashe
Published at 06:17 AM Apr 18 2024
Mpira ukiwa golini.
Picha: Maktaba
Mpira ukiwa golini.

TIMU ya Uhamiaji FC imesema matarajio na mipango yao ya kumaliza nafasi nne za juu katika msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar msimu huu, yanategemea zaidi kufanya vizuri michezo 10 ya ligi hiyo ambayo inatarajiwa kuendelea Aprili 27, mwaka huu, baada ya kusimama kwa muda.

Uhamiaji FC ni miongoni mwa timu ambazo zimevuna alama moja moja mara nyingi kutokana na kupata sare 10 katika mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Abdisaleh Abdallah, alisema baada ya kutopata matokeo ya kuridhisha karibia nusu ya michezo waliyocheza msimu huu, michezo iliyobakia wamejipanga  kuhakikisha wanashinda ili kuiweka timu yao katika nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Alisema katika kuhakikisha wanatimiza ndoto yao hiyo, kwa sasa baada ya kumaliza mfungo wa Ramadhani ameandaa programu maalum ya kuwajenga kimwili wachezaji  wake 'fitness' kutokana na mapumziko ya muda mrefu waliyoyapata.

Alisema mpango huo unalenga kuwarejesha mchezoni wachezaji pamoja na kuyanfanyia kazi mapungufu waliyoyaona katika michezo iliyopita.

Alisema eneo kubwa ambalo watalifanyia kazi ni nafasi ya  ushambuliaji pamoja na mabeki wa kulia kwa kuwa idara hizo mara kwa mara zimekuwa zikifanya makosa yanayojirudia.

“Tunarudi na kasi kubwa, kasi ambayo tunataka kufanikisha lengo letu la kunyakuwa alama tatu katika kila mchezo ambao tunashuka uwanjani,” alisema.

Aidha, alisema katika mchezo wao wa kirafiki dhidi ya Klabu ya Simba, waliweza kupata mbinu mpya ambazo watazitumia vizuri hasa kwa upande wa washambuliaji na walinzi.

Alisema anaamini kupitia mchezo huo wa kirafiki na michezo kadhaa waliyocheza itawasaidia katika kufanikisha lengo lao la kupata matokeo ya ushindi katika mechi 10 zilizobaki.

Timu ya Uhamiani FC ipo nafasi ya saba ikiwa na alama 28, katika michezo 20 iliyocheza hadi sasa katika ligi hiyo ikiwa imeshinda mechi sita, sare 10 na kufungwa mara nne.