Utakatifu sana wa Kaka umefanya mke aombe talaka

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:31 AM Apr 15 2024
news
Picha: Wikipedia
Mchezaji wa zamani wa Kimataifa wa Brazil, Kaka, akiwa na mke wake wa zamani Caroline Celico.

MKE wa zamani wa mchezaji wa Kimataifa wa Brazil, Kaka, amefichua sababu ya ajabu iliyomfanya kuomba talaka mwaka 2015 baada ya miaka 10 ya ndoa yao, kwamba mume wake alikuwa mtakatifu sana.

Kaka mwenye umri wa miaka 41, alifurahia maisha mazuri katika Klabu za Sao Paulo, AC Milan, Real Madrid na Orlando City, kabla ya kustaafu mwaka 2017.

Mnamo mwaka 2005, wakati alipokuwa aking'ara AC Milan, Kaka alifunga ndoa na mpenzi wake wa utotoni, Caroline Celico.

Katika ndoa yao wana Watoto wawili, wa kiume na wa kike, lakini walitangaza kwenye mitandao ya kijamii kuwa walitengana mnamo 2015 baada ya miaka 10 ya ndoa.

Na, kama ilivyoripotiwa na gazeti la The Sun, Celico ambaye ameolewa tena - alielezea kwa nini aliamua kutengana na mumewe.

“Kaka hakuwahi kunisaliti,” alisema. 

“Alinitendea vizuri, alinipa familia nzuri, lakini sikuwa na furaha, kuna kitu kilikosekana.

“Tatizo lilililokuwapo ni kwamba, Kaka alikuwa mkamilifu sana kwangu (mtakatifu mno).”

Kaka anajulikana kama Mkristo mwaminifu mno na wakati wa ndoa yao Celico alijiunga na kanisa la nyota huyo wa soka, kabla ya kuwa mchungaji wa Kiinjili.

Aliacha jukumu hilo mwaka wa 2010 na kuanzisha Horizontal Love, shirika la hisani ambalo hutoa vifaa vya chakula, usafi, ujenzi na elimu kwa mashirika yasiyo ya kiserikali ya Brazil.

Baada ya kutengana kwao, Kaka sasa anaishi na mpenzi wake mpya Carolina Dias tangu mwaka 2017.

Wawili hao walitangaza uchumba mapema mwaka huu, huku Kaka pia akiwa na mtoto wa kike mwenye umri wa mwaka mmoja na mwanamitindo huyo wa Brazil.

Maisha ya Kaka yaliyopambwa sana kwenye mchezo huo yalimfanya kushinda mataji 12, likiwamo Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kombe la Dunia, huku pia akifunga mara 29 katika mechi 92 alizoichezea Brazil.