Viwanja AFCON 2027 kukamilika mwakani

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 10:32 AM May 22 2024
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma.
Picha: Bungeni
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma.

BUNGE limeelezwa ujenzi wa viwanja vipya vya michezo kwa ajili ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), vinatarajiwa kukamilika mwakani ili kupisha ukaguzi wa kikanuni utakaofanywa na maofisa wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma, amesema hayo bungeni jana alipokuwa akijibu swali la nyongeza Mbunge wa Chakechake, Ramadhan Suleiman Ramadhan, ambaye amehoji lini viwanja vipya ambavyo serikali inatarajia kujenga kwa ajili ya matayarisho ya AFCON vitakamilika. 

Mwinjuma akijibu swali hilo, alisema kwa mujibu wa ratiba na mahitaji, viwanja hivyo vinatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka ujao ili kupisha ukaguzi wa kikanuni wa CAF ambao utafanyika baada mwaka 2025.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Chumbuni, Ussi Salum Pendeza, amehoji ni lini serikali itaamua kuwekeza kwa nguvu zote katika viwanja, walimu na mawakala wa michezo mbalimbali inayoonekana kuleta tija kwa Taifa.

Akijibu swali hilo, Mwinjuma, alisema serikali inatekeleza ujenzi wa viwanja vya mpira wa miguu katika mikoa ya Arusha, Dodoma, Zanzibar (Fumba), Ilemela jijini Mwanza pamoja na akademia na hosteli katika Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya.

CAF tayari imeshatangaza rasmi Tanzania, Kenya na Uganda zitakuwa wenyeji wa Fainali za AFCON zitakazofanyika mwaka 2027, 

Nchi hizo tatu za Afrika Mashariki zimepata nafasi hiyo baada ya kupeleka maombi ya pamoja.

Hata hivyo, Tanzania pia inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), zitakazochezwa Septemba, mwaka huu.

Uwanja wa Benjamin Mkapa, Uhuru na Azam Complex, vinatarajiwa kufungwa ili kupisha maboresho kwa ajili ya kukidhi viwango vya mashindano hayo ya kimataifa.