Utafanyaje pale ugunduapo cheti cha ndoa yako ni batili?

By BBC Swahili , Agency
Published at 11:01 AM Mar 24 2024
Wanandoa wakipiga picha ya kumbukumbu.
Picha: Getty Images
Wanandoa wakipiga picha ya kumbukumbu.

SINTOFAHAMU yawakumba maelfu ya wanandoa wapya nchini Zimbabwe, baada ya kugundua kuwa vyeti vyao vya ndoa ni batili.

Watu hao waliooana hivi karibuni nchini humo, wameshangaa kujua kwamba vyeti vyao vya ndoa si halali.

Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) limeripoti sababu batili huo ambao unahusisha vyeti vilivyotolewa ndani ya miezi 18 iliyopita kuwa ni la kiufundi, jambo ambalo linaweza kuathiri wanandoa wote waliofunga ndoa ndani ya kipindi hicho.

Kwa mujibu wa BBC, ubatili huo wa vyeti unajulikana kipindi ambacho Chama cha Wanasheria cha Zimbabwe (LSZ), kikitoa notisi ya tahadhari kwa wanasheria wote nchini humo.

LSZ imebainisha kuwa vifaa vya kuandikia vinavyotumika kwenye vyeti hivyo vya ndoa za kiraia, vinaendelea kunukuu sura ya sheria ya zamani ya ndoa ambayo ilibatilishwa mwaka 2022.

Sheria mpya, ambayo ilianza kutumika Septemba 2022, ilileta mabadiliko makubwa, ikiwa ni pamoja na haki kwa wapenzi katika ndoa za kimila. Pia iliharamisha ndoa za utotoni.

Chama cha wanasheria kimewashauri walioathirika kupeleka vyeti vyao kwa msajili ambaye atarekebisha na kugonga muhuri wa hati hiyo.

Wanasheria pia walionya ikiwa una cheti batili huwezi kupata talaka.

Wapenzi kadhaa waliooana hivi karibuni ambao walizungumza na BBC hawakujua hapo awali kwamba vyeti vyao vinaweza kuwa batili.

Mkanganyiko huo uliibua gumzo kwenye majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kijamii, huku wengine wakitania ilikuwa fursa kwa wale wanaotafuta njia ya kutoka nje ya ndoa zao.

Idara ya Usajili wa Kiraia iliambia jarida linalomilikiwa na serikali The Chronicle kwamba ingawa inaweza kurekebisha vyeti vilivyopo, haiwezi kuchapisha maandishi mapya yenye sheria sahihi bila serikali kwanza kutangaza mabadiliko hayo kupitia gazeti la serikali.

Chanzo BBC