Al Ahly yavunja rekodi ya Simba

By Adam Fungamwango ,, Saada Akida , Nipashe Jumapili
Published at 04:37 PM Mar 31 2024
Mshambuliaji wa Simba, Kibu Denis (kushoto), akijipanga kumtoka beki wa Al Ahly kutoka Misri katika mechi ya hatua ya  robo fainali ya mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam juzi usiku
PICHA: SIMBA SC
Mshambuliaji wa Simba, Kibu Denis (kushoto), akijipanga kumtoka beki wa Al Ahly kutoka Misri katika mechi ya hatua ya robo fainali ya mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam juzi usiku

WAKATI ushindi wa bao 1-0 walioupata Al Ahly kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam juzi usiku umehitimisha rekodi nzuri ya Simba nyumbani, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Abdelhak Benchikha, amesema washambuliaji wake walimwangusha katika mechi hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba juzi imepoteza mechi ya kwanza ya mashindano ya kimataifa dhidi ya Waarabu hao kutoka Misri.

Lilikuwa ni bao la dakika ya nne likifungwa na Ahmed Nabil Koka, lilihitimisha rekodi nzuri ya Simba, lakini pia likiiweka katika  nafasi ngumu kuelekea mechi ya marudiano ya robo ya michuano hiyo itakayochezwa Ijumaa kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo.

Simba ilikuwa haijawahi kupoteza mechi yoyote dhidi ya Al Ahly ikicheza nyumbani, lakini rekodi hiyo ilifikia kikomo juzi baada ya michezo tisa, tangu zilipokutana mara ya kwanza mwaka 1985.

Simba ilianza kucheza na Al Ahly Agosti 22, 1985 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini, Mwanza ikashinda mabao 2-1, ikiwa ni michuano ya Kombe la Washindi Afrika, sasa Kombe la Shirikisho, lakini ikatolewa kwa kufungwa magoli 2-0 ugenini, mechi ikifanyika Agosti 29, mwaka huo.

Februari 2, mwaka 2019 katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi, Simba ilifungwa mabao 5-0 ugenini, kabla ya kushinda goli 1-0 nyumbani, siku 10 baadaye.

Simba ilishinda tena nyumbani dhidi ya Al Ahly bao 1-0 hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa, Fabruari 23, mwaka 2021, lakini ikaenda kufungwa bao 1-0 ugenini Aprili 9, mwaka huo.

Kwa mara ya kwanza Simba ilitoa sare nyumbani ya mabao 2-2 dhidi ya Al Ahly, Oktoba 20, mwaka jana kwenye michuano ya African Football League, ikapata sare ya kwanza ugenini dhidi ya timu hiyo (1-1), Oktoba 24, mwaka jana.

Baada ya mechi hiyo kumalizika juzi, Benchikha amesema licha ya kufurahia kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wake, lakini alilalamika kukosa mabao saba ya wazi katika mchezo huo.  

"Tumecheza dhidi ya timu kubwa, tumefanya kosa moja wametufunga, wamepata nafasi moja wameitumia, kwa ujumla tumecheza mechi nzuri na tumecheza vizuri, lakini hatukufunga. Kama hufungi huwezi kushinda, lakini tuna mechi ya marudiano, hatuna cha kupoteza.

Katika mechi kubwa hizi huwezi kupata nafasi nyingi kama hizi, niombe radhi ya mashabiki kwa sababu kama hakuna matokeo mazuri ni tatizo. Niseme tu tuna matatizo, kama wachezaji wanaingia ndani ya eneo la hatari mara saba na mnashindwa kufunga ni tatizo," Benchikha amelalamika.

Ameongeza wachezaji wake walipambana na wamejaribu kucheza vizuri dhidi ya vigogo hao wa Afrika.

"Wachezaji wote wamecheza vizuri, Ngoma (Fabrice), Ntibazonkiza (Said), Kibu (Dennis), wachezaji wote wamecheza vizuri. Kuna mchezo wa pili, hatuna cha kupoteza tunajiandaa kucheza mchezo wetu mkubwa, na leo (juzi), wachezaji wangu wamekuwa na mchezo mzuri, unapochezea dhidi ya timu kubwa, tumeruhusu bao dakika za mwanzoni,” amesema Benchikha.

Naye aliyekuwa Kocha Msaidizi wa Simba, Juma Mgunda, amesema wamecheza mpira mzuri lakini bao la mapema walilopata Al Ahly lilimaliza mchezo.

“Kwa jinsi tulivyocheza, tumemiliki mpira na kutengeneza nafasi zaidi ya sita lakini tatizo ni umakini wa washambuliaji kushindwa kufunga, ninaimani kubwa ndani ya siku tatu hizi benchi la ufundi litafanyia kazi na kwenda Misri kwa matumaini makubwa,” amesema Mgunda.

Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji, amesema anaona nafasi kubwa ya timu zote za Tanzania kutinga hatua ya nusu fainali, licha ya Simba kupoteza mchezo wa nyumbani.

“Mpira ni mchezo wa makosa, hii mechi hajapoteza Simba pekee, Tanzania kwa sababu ilikuwa uwanjani kuipeperusha bendera ya nchi, ninaimani nao wanaenda kufanya maajabu Misri,  na timu zote zinaweza kwenda nusu fainali,” amesema bosi huyo wa Yanga.

Kocha Mkuu wa Al Ahly,  Marcel Koller, alifurahi kwa ushindi na alifahamu mchezo huo utakuwa mgumu kutokana na baadhi ya wachezaji wametoka katika majukumu ya timu za taifa na wakalazimika kusafiri moja kwa moja bila kupata muda wa kupunzika.

“Mchezo ulikuwa mgumu, huu umeisha na sasa tunahamisha macho yetu mchezo wa marudiano, utakuwa mgumu na tofauti kwa sababu bado hatujashinda, tunaongoza tu,” amesema Koller.