Azam FC, Mtibwa hapatoshi FA Cup

By Saada Akida , Nipashe Jumapili
Published at 02:59 PM Apr 07 2024
Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssouph Dabo.
PICHA: AZAM FC
Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssouph Dabo.

AZAM FC inatarajia kuikaribisha Mtibwa Sugar katika mechi ya hatua ya 16 Bora ya mashindano ya Kombe la CRBD Bank FA itakayochezwa leo kuanzia saa 3:00 usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Timu hizo zinakutana kwa mara ya tatu katika msimu huu, mara mbili katika Ligi Kuu Tanzania Bara ambazo zote Azam iliondoka na ushindi.

Tayari Namungo FC, Geita Gold FC, Tabora United na Coastal Union zimeshatinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo. 

Akizungumza na gazeti hili, Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssouph Dabo, amesema timu yake imejiandaa vyema kuelekea mchezo huo na anaamini hautakuwa rahisi licha ya kuwafunga Mtibwa kwenye michezo yote ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Dabo amesema hawatawadharau wapinzani wao kwa sababu anafahamu leo wataingia na mbinu tofauti baada ya kujiimarisha kwa kufanyia kazi mapungufu yao.

“Tunaenda katika mchezo wa mtoano ambao kila timu inahitaji kutafuta ushindi kwa ajili ya kusonga mbele, tutapambana ili kupata ushindi, tuko tayari kwa mechi hii,” amesema Dabo.

Naye Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila, amesema akiandaa vizuri kikosi chake na anataka kutumia mashindano hayo kuwafurahisha mashabiki wao kutokana na kutofanya vyema katika michezo ya Ligi Kuu msimu huu.

Katwila amesema anatambua ubora wa Azam na ili kuvuna matokaeo chanya, amewaandaa wachezaji wake kupambana na kuhakikisha wanaiondoa Azam katika michuano hiyo.

“Hakuna mechi rahisi katika mashindano haya ya mtoano, timu zote zilizofika hatua hii ni bora, na kila mmoja anatamani kuona atafuzu hatua ya robo fainali, tutaenda kupambana kwa wakati wote,” Katwila amesema.

Aliongeza kwa kuwataka washambuliaji wake kuongeza utulivu huku mabeki kuimarisha safu yao ili kutoruhusu wenyeji kutawala mchezo huo.