Benchikha awapa wachezaji mapumziko maalum Z'bar

By Saada Akida , Nipashe Jumapili
Published at 02:40 PM Mar 24 2024
Kocha wa Simba Abdelhak Benchikha.
PICHA: SIMBA SC.
Kocha wa Simba Abdelhak Benchikha.

WAKATI wakiendelea kujifua kuelekea kwenye mchezo wao wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wachezaji wa Simba wametengewa muda maalum wa mapumziko.

Akizungumza na Nipashe kutoka Zanzibar walipoweka kambi, Kocha wa timu hiyo, Abdelhak Benchikha amesema licha ya mchezo mgumu walionao wiki ijayo amewataka wachezaji wake kuwa na muda wa kupumzisha akili zao na kujielekeza sana kwenye mchezo huo dhidi ya Al Ahly. 

Benchikha, amesema mechi dhidi ya Al Ahly ni mchezo muhimu na wanatambua ubora wa Al Ahly, lakini wachezaji wake hawatakiwi kuhofia zaidi ya kujiweka na kuufikiria mchezo huo na jinsi ya kwenda kupambana na kutafuta ushindi siku hiyo ya Ijumaa.

Amesema licha ya kufanya mazoezi mara mbili kwa siku lakini ametenga muda maalum kwa ajili ya wachezaji wake kupumzisha akili zao ziwaze mchezo huo tu.

Amesema kulingana na programu zake kuelekea mchezo huo, kambi ya Zanzibar inawasaidia hasa wachezaji wake kulingana na mazingira ya kufanyia kazi na kuwataka kusahau yote na kutambua umuhimu wa mchezo dhidi ya Al Ahly. 

“Tunahitaji kufanya mazoezi mara mbili kwa siku asubuhi na usiku, lakini pia wachezaji kupata muda wa kupumzisha akili yao kujielekeza zaidi katika mchezo wetu muhimu.

"Tunafahamu ubora wa Al Ahly na tumecheza nao mara kadhaa na mara ya mwisho tulionyeshana ushindani na ninaamini wachezaji wanapotuliza akili na kupambana zaidi kwa kufuata maelekezo watafanikiwa kupata matokeo mazuri ya ushindi,” amesema Benchikha. 

Ameongeza kuwa  amekuwa akifanya kikao  na wachezaji wake na kuwaeleza mipango na umuhimu wa mchezo huo ambapo baadhi ya nyota wa timu hiyo ni mara yao ya kwanza kucheza hatua hiyo.

Katika hatua nyingine, kiungo  Mshambuliaji wa timu hiyo, Willy Essomba Onana, amesema huu ni wakati muhimu kwa timu yake kwenda kuandika historia mpya barani Afrika kwa kutinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza.

Amesema anajua wanaenda kupambana na bingwa mtetezi hivyo hautakuwa mchezo rahisi kwao lakini ndio wakati wa kwenda kuonyesha ubora wao kwa kutimiza malengo yao ya muda mrefu.

“Binafsi najisikia vizuri kucheza robo fainali kwa mara ya kwanza, Al Ahly ni kama Real Madrid kwa Afrika inaweza kuwa kwenye kipindi cha mpito lakini kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa wanakuja kivingine.

“Hivyo tunajua tunaenda kucheza na timu kubwa sana Afrika hizi ni nyakati bora kwa wachezaji na viongozi wa benchi la ufundi  kuandika historia mpya,” amesema Onana.

Amesema alikuwa akiingalia Simba ikiishia hatua ya robo fainali lakini ni wakati wa kwenda kubadili historia.