Mabao ya 'usiku' tatizo Geita

By Adam Fungamwango , Nipashe Jumapili
Published at 07:34 PM Feb 18 2024
Geita Gold FC
PICHA :Na Mtandao
Geita Gold FC

KOCHA Mkuu wa Geita Gold FC, Denis Kitambi, amesema wachezaji wake wanaonekana kukosa umakini katika dakika 10 za mwisho katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara, ambapo nyota wake wamekuwa wakiruhusu mabao.

"Mechi ya pili tunaruhusu goli katika dakika 10 za mchezo ni lazima tukifanyie kazi, ni ukosefu wa umakini, na nimeona pia katika mechi zote mbili pia mabao yote tunafungwa ya krosi, inabidi sasa tufanyie kazi, tunagalie ni namna gani tunajilinda dhidi ya krosi," amesema Kocha Kitambi.

Mara baada ya kumalizika kwa mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa juzi dhidi ya Azam FC, Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam na kufungwa mabao 2-1, Kitambi alilia na safu yake ya ulinzi akisema wanakosa umakini, hali ambayo inawafanya wapoteze pointi.

Katika mechi ya juzi, Geita Gold iliruhusu bao la kwanza dakika moja kabla ya mapumziko, likifungwa na Gilbril Sillah huku goli la pili likiwekwa wavuni na Idd Nado dakika saba kabla ya mechi kumalizika wakati wao walipata bao la kufutia machozi likifungwa na Tariq Seif.

Jumatatu iliyopita kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Geita Gold iliruhusu bao dakika tisa kabla ya mechi kumalizika likifungwa na Babakar Sarr na hivyo Simba kuondoka na pointi tatu.

Kitambi amesema wachezaji wake wamefanya makosa hayo katika mechi mbili zilizopita na pia amebaini mabao yote waliyoruhusu ni ya krosi.

"Mechi ya pili tunaruhusu goli katika dakika 10 za mchezo ni lazima tukifanyie kazi, ni ukosefu wa umakini, na nimeona pia katika mechi zote mbili pia mabao yote tunafungwa ya krosi, inabidi sasa tufanyie kazi, tunagalie ni namna gani tunajilinda dhidi ya krosi," amesema Kitambi.

Hata hivyo, kocha huyo ameonyesha kufurahishwa na kiwango cha wachezaji wake katika mechi ya juzi tofauti na walipocheza dhidi ya Simba.

"Leo (juzi), angalau tumeweza kumiliki mpira, wachezaji wangu 'mali' ilikuwa inakaa mguuni tofauti na mechi dhidi ya Simba ambapo walionekana wana wasiwasi, tunaangalia sasa tuendelee kujenga kutokana na hiki tulichokipata na kukiona," Kitambi amesema.