Morocco afurahia upambanaji Taifa Stars

By Saada Akida , Nipashe Jumapili
Published at 05:00 PM Mar 24 2024
Kocha Mkuu wa timu ya taifa 'Taifa Stars', Hemed Suleiman 'Morocco'.
PICHA: TMICHEZO
Kocha Mkuu wa timu ya taifa 'Taifa Stars', Hemed Suleiman 'Morocco'.

LICHA ya kupoteza mchezo wa juzi dhidi ya Bulagaria kwa kubali kipigo cha bao 1-0, Kaimu Kocha Mkuu wa timu ya taifa 'Taifa Stars', Hemed Suleiman 'Morocco' amesema amefurahishwa na hali ya upambanaji iliyoonyeshwa na wachezaji na ana matumaini ya kupata ushindi kwenye mchezo wao wa leo katika michuano hiyo maalum ya FIFA 'FIFA Series 2024'.

Taifs Stars leo inashuka tena kwenye uwanja wa Dalga katika mji wa Baku nchini Azerbaijan kuumana na Mongolia.

Akizungumza na Nipashe , Morocco alisema  kitu cha faraja kwake ni kuona kuna hali ya upambanaji imeongezeka ndani ya kikosi na kama benchi la ufundi watajitahidi kukazia hapo ili kufanya wachezaji waimarike zaidi.

Amesema sio rahisi kwa hali ya hewa waliyokutana nayo nchini humo  wachezaji kuwa na muendelezo mzuri kwa dakika zote 90.

“Tumeona mapungufu tunayafanyia kazi, tutaweza kufanya vizuri zaidi kama tukipata muda, lakini  hata hali ya hewa imekuwa chanzo cha kupoteza mchezo, kwa kuwa tulipata nafasi ya kujaribu kuisukuma timu mbele ilikuwa inaonekana kuna kitu tungeweza kufanya kama tungekuwa makini kidogo," amesema Morocco.

Ameongeza kuwa vijana wake waliweza kumiliki mpira kama ilivyo falsafa yake na anaamini kama wataendelea kufanya hivyo na kutengeneza nafasi nyingi wanaweza kufanya vizuri kwenye mchezo wa leo.

“Tunahitaji kufanya mazoezi zaidi ili tuweze kupata muendelezo wa kiwango hiki kwa muda mwingi wa kumiliki mpira, wachezaji wote wanalingana lakini tunahitaji kuongeza hali ya  kupambana zaidi, tumeona makosa yetu kwenye mchezo wa jana (juzi), naamini kwenye mchezo ujao (leo) tutafanya vizuri zaidi," amesema kocha huyo.

Kwa upande wake, nahodha wa kikosi hicho kilichopo kwenye michuano hiyo, Himid Mao amesema mpira ni mchezo wa nafasi hivyo inapopatikana nafasi ni lazima waitumie na kuendelea kujifunza.

“Mechi ilikuwa imegawanyika asilimia 50 kwa 50 wao walikuwa na nafasi na sisi tulikuwa na nafasi, katika nafasi walizopata moja wakaitumia ila matokeo yalikuwa sawa kabisa, kama wachezaji na benchi zima la ufundi wameona nini kilikosekana pale tutaenda kwenye uwanja wa mazoezi kurekebisha kwa ajili ya michezo inayokuja,” amesema Himid.