Mshambuliaji wa KMC bado aitamani Yanga

By Adam Fungamwango , Nipashe Jumapili
Published at 03:26 PM Apr 07 2024
Mshambuliaji wa KMC FC, Waziri Junior.
PICHA: MAKTABA
Mshambuliaji wa KMC FC, Waziri Junior.

MSHAMBULIAJI wa KMC FC, Waziri Junior, ambaye aliwahi kuichezea Yanga, amesema iwapo angepewa muda na kuvumiliwa, basi saa hizi klabu hiyo ingekuwa inakula matunda yake kwa kuwafungia 'mabao muhimu' katika mechi mbalimbali za Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya kimataifa.

Waziri Jr amefunga mabao 11 mpaka sasa akiwa katika nafasi ya pili kwenye orodha ya wafungaji bora nyuma ya Stephane Aziz Ki wa Yanga na Feisal Salum 'Fei Toto' wa Azam FC wenye mabao 13 kila mmoja.

Akizungumza na gazeti hili , Waziri Jr, amesema kama aliyekuwa Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, angebaki katika kikosi hicho, anaamini angepata nafasi ya kufanya makubwa na anadhani angekuwepo hadi leo hii.

Nyota huyo amepinga mawazo ya baadhi ya mashabiki wanaodai yeye ni mchezaji wa daraja la kati tu na si la juu, hivyo hawezi kung'ara katika klabu kubwa, badala yake ataendelea kuwika kwenye klabu ndogo kama KMC anayochezea sasa.

“Unasajili mchezaji humpi nafasi ya kucheza, au unampa mechi chache utasema huyo mchezaji ni wa daraja la kati? Kocha, Cadric Kaze alinipa nafasi katika mechi tatu nikafunga goli moja," amesema straika huyo.

Amemsifu pia Nabi kuwa ndiye kocha aliyempa nafasi na kumfanya awe bora, na hata alipotoka, mazoezi yake yamemfanya awe mchezaji mzuri akiwa KMC.

“Nabi ndiyo mtu aliyenipa nafasi mpaka msimu unaisha, mwalimu ndiyo atamfanya mchezaji awe bora, angebaki ningefanya makubwa ndani ya Yanga,”  Waziri Jr amesema.

Mchezaji huyo ambaye pia ameshawahi kuicheza Azam FC, aliondoka Yanga mwaka 2021, na alitua Jangwani akitokea Mbao FC ya jijini, Mwanza.