Simba SC yatamba haiishi mpaka iishe

By Saada Akida ,, Adam Fungamwango , Nipashe Jumapili
Published at 01:14 PM May 05 2024
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally.
PICHA: SIMBA SC
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally.

WAKATI uongozi wa Simba ukisema bado hawajakata tamaa ya kukata tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa msimu ujao, winga chipukizi wa timu hiyo, Saleh Karabaka, ambaye alifunga bao lake la kwanza juzi amefunguka alichokifanya uwanjani ni 'matunda' kutoka kwa Kaimu Kocha Mkuu, Juma Mgunda.

Simba ilipata ushindi wake wa kwanza tangu Machi 15, mwaka huu, kwa kuifunga Mtibwa Sugar mabao 2-0, mechi iliyochezwa  kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, shukrani Fred Michael na Karabaka.

Ushindi huo ulianza kufufua matumaini ya Simba kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

Akizungumza na gazeti hili, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema kwa sasa wanaamini  watamaliza msimu katika moja kati ya nafasi mbili za juu ili kurejea tena kwenye mashindano ya kimataifa msimu ujao.

"Kwanza ulikuwa ushindi muhimu ili wachezaji wetu waanze kujisikia vizuri, unajua timu isipopata ushindi, wanaoanza kuathirika ni wachezaji. Pili ni tulikuwa tunahitaji ushindi kwa ajili ya kurudisha imani kwa mashabiki wetu, tatu bado tunasaka nafasi mbili za juu, ubingwa au nafasi ya pili, hatujakata tamaa, tunazidi kupambana, haiishi mpaka iishe," amesema Ahmed.

Nyota wa zamani wa JKU ya Zanzibar,  Karabaka, ambaye alifunga bao la pili katika mchezo huo wa juzi amesema kabla ya kuingia uwanjani kama mchezaji wa akiba kipindi cha pili, aliteta na Mgunda.  

"Mwalimu (Mgunda), aliniita na kuniambia timu haikimbii, yaani wachezaji wetu wanakwenda langoni kwa wapinzani bila kasi yoyote, akaniambia ili hawa tuwafunge, tuwe tunakimbia muda wote, tukikamata mpira tusiangalie nyuma, sisi ni mbele tu muda wote, nilivyoingia mimi na wachezaji wenzangu wa akiba tukatekeleza majukumu, tukaondoka na ushindi," amesema Karabaka.

Naye Mgunda amesema timu yao bado inaendelea kujipanga kuhakikisha inamaliza msimu kwa kupata matokeo chanya.

"Kwa sasa tunachohitaji ni kushinda michezo yetu, mwisho wa siku ndiyo tutaona tutakuwa tumesimamia wapi, lakini hatujakata tamaa na ubingwa la wala nafasi ya pili, mshindi wa mbio za marathoni anapatikana pale anapogusa na kukata utepe, na si vinginevyo," amesema Mgunda.

Kuhusu kutoa nafasi kwa wachezaji vijana, Mgunda amesema mchezaji yoyote aliyesajiliwa na Simba lazima anakuwa na uwezo, klabu kama hiyo haiwezi kusajili ili mradi tu, hivyo anatakiwa kuitumikia.

"Katika mechi hii, tulicheza na timu ambayo haijalishi matokeo waliyonayo, ila uwezo waliokuwa nao, wana uwezo mkubwa, wana vijana wazuri wenye vipaji, ila tunashukuru kwa kupata pointi tatu, hii imekwisha tunajipanga na mchezo ujao," Mgunda amesema.

Hata hivyo, Simba inaendelea kushika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 50 nyuma ya vinara Yanga yenye pointi 62 na Azam FC yenye alama 54 kibindoni.

Simba itashuka tena dimbani kusaka pointi tatu muhimu za Ligi Kuu Tanzania Bara kesho kwa kuwakaribisha Tabora United na Mei 9, mwaka huu itakutana na Azam FC kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.