Ugumu makocha weusi kuajiriwa Ulaya - utafiti wabainisha kiini

By BBC Swahili , Agency
Published at 11:57 AM Mar 24 2024
Vincent Kompany (kushoto), kocha wa Burnley, na yule wa Nottingham Forest, Nuno Espírito Santo ndio mameneja wawili pekee wa Ligi Kuu ya Uingereza ambao ni weusi.
Picha: Getty Images
Vincent Kompany (kushoto), kocha wa Burnley, na yule wa Nottingham Forest, Nuno Espírito Santo ndio mameneja wawili pekee wa Ligi Kuu ya Uingereza ambao ni weusi.

TAASISI ya Black Footballers Partnership (BFP), imesema wachezaji wasio weusi wana uwezekano wa hadi asilimia 50 kupata ukocha katika timu kuliko wachezaji weusi katika kipindi cha miaka 30.

Hii ni kwa mujibu wa utafiti walioufanya ambao uliangazia maisha ya nje ya uwanja ya takribani wanasoka 3,500 wa zamani waliocheza Ligi Kuu ya Uingereza au Klabu Bingwa kati ya 1990 na 2010.

Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) limeripoti kuwa utafiti huo uliofanywa na wasomi watatu, umegundua kuwa licha ya wachezaji weusi kuwa na asilimia 25 ya sifa za ukocha kama zilivyotolewa na Uefa, mwaka 2022 na 2023, ni asilimia nne tu ya wachezaji hao, ndiyo wamechangia katika majukumu ya ukocha.

Delroy Corinaldi, mkurugenzi mtendaji wa BFP, anasema: "Kazi katika usimamizi wa soka mara nyingi inaonekana ni kazi inayoongeza watu, lakini kwa wachezaji wa zamani weusi, hawaongezeki katika kazi hiyo".

BFP ni taasisi ya wachezaji weusi waliopo na wa zamani.

Ripoti hiyo imetoa muhtasari kwamba wachezaji wa zamani weusi hupata nafasi chache kwenye usimamizi, na kwamba hupandishwa vyeo polepole zaidi, jambo ambalo pia hudumaza maendeleo yao na hivyo kufukuzwa kazi haraka kuliko wenzao wasio weusi.

Pia ripoti hiyo imeeleza mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na:

Kocha mweusi ana uwezekano wa asilimia 41 kufutwa kazi kuliko kocha mzungu - wakati vipengele kama vile utendakazi ni sawa. Na katika majukumu yote ya usimamizi, mtu mweusi ana uwezekano wa asilimia 17 kufutwa kazi.

Kati ya wachezaji 3,500 katika utafiti huo, asilimia 73 ya wachezaji weusi walicheza Ligi Kuu ya Uingereza kwa wastani wa mechi 62 kwa kila mchezaji, huku asilimia 62 ya wachezaji wasio weusi walionekana kwenye ligi kuu, na wastani wa mechi 49.

"Matokeo ni ya kushangaza sana," Corinaldi ameliambia shirika la habari la PA.

"Wachezaji kandanda wamekuwa kizazi kilichopotea nje ya uwanja, licha ya kuwa walikuwa nyota ndani ya uwanja."

Ripoti hiyo ilichapishwa muda mfupi baada ya kuthibitishwa kuwa serikali ya Uingereza itaanzisha msimamizi huru wa soka wakati Mswada wa Utawala wa Soka utakapowasilishwa Bungeni siku ya Jumanne.

Wachezaji wa zamani wakiwemo Les Ferdinand, Chris Ramsey, Michael Johnson, Ricky Hill, Paul Davis na Sol Campbell wamejiunga na wito wa Corinaldi – kutaka malengo ya ushirikishwaji na ujumuishwaji wa watu wa jamii mbalimbali yawemo katika Mswada wa Utawala wa Soka.

Pia wametoa wito kwa wadau wa soka kufanya kazi na BFP ili kuelewa ubaguzi katika mchezo huo na kwa wanasoka weusi kupata msaada wanaohitaji ili kujiendeleza kila ngazi ya mchezo bila kuzuiwa na chuki au ubaguzi wa rangi.

"Mdhibiti huru anaweza kutoa fursa lakini ikiwa hatashughulikia usawa wa rangi katika mchezo kulingana na data zinavyoonyesha basi itakuwa ni fursa iliyokwenda bure," aliongeza Corinaldi.

"Ripoti hii ni fursa kwa mchezo wa soka kujiunda upya, kushirikiana tena na BFP ili tufanye kazi kuelekea suluhisho endelevu."