GGML yapongezwa kudhibiti vifo kazini

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:15 AM May 01 2024
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko.
Picha: Mpigapicha Wetu
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko.

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, ameipongeza Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa kudhibiti matukio ya vifo na majeruhi katika shughuli za uchimbaji mgodini na kuwataka waajiri wengine kulinda usalama wa waajiriwa wao.

Dk. Biteko alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita  baada ya kutembelea banda la GGML katika maonesho ya afya na usalama mahali pa kazi yanayoendelea Viwanja vya General Tyre jijini Arusha.

Biteko ambaye pia alikuwa mgeni rasmi katika kilele cha maonesho hayo, alieleza kufurahishwa na elimu ya afya na usalama mahali pa kazi inayotolewa na washiriki.

“Niwapongeze wale mliofanya maonesho hapa, mmetoa elimu kubwa kwangu na kwale ambao tumepita, lakini tumejifunza bado zipo kazi za kufanya,” alisema.

Alisema waajiriwa wanatakiwa kuzingatia usalama na afya mahali pa kazi kwani kifo cha mtu mmoja kwa takwimu ni sawa na asilimia 100 kwa wategemezi wake ambao ni mke, watoto, ndugu na majirani.

“Kifo cha mtu mmoja ni kikubwa, kinatakiwa kisitokee. Wito kwa waajiri wote wakati wote ninataka mhakikishe mnarekodi sifuri katika matukio haya ya vifo mahali pa kazi. 

“Kwa waajiriwa wito wangu kwenu ni kwamba mtu wa kwanza kulinda usalama ni mwajiriwa mwenyewe, ukiona mtambo unaopaswa kuundesha na una kasoro huku ukiwa umelazimishwa na mwajiri kuuendesha, uwe wa kwanza kusema mtambo huu haupo salama na usihesabike kuwa mtu uliyegoma kwa sababu pia una wajibu kulinda usalama wako,” alisema.

Alitoa wito kwa kila mtu kuthamini maisha yake pindi anapokuja kazini anarejea salama bila kuwa na madhara yoyote.

Awali akimkaribisha Dk. Biteko katika banda la GGML, Meneja Usalama wa kampuni hiyo, Isack Senya alisema kuwa kwa kipindi cha zaidi ya miaka 15 halijatokea tukio la vifo kwa mfanyakazi akiwa kazini.

“Tuna miaka zaidi ya sita hakuna mtu aliyeumia akashindwa kurudi kazini siku inayofuata. Suala la msingi  tunajitahidi kujifunza kwa wenzetu na kuendelea kuboresha mazingira ya afya na usalama mahali pa kazi,” alisema.

Senya alimwelezea Dk. Biteko namna GGML inavyotumia mfumo wa rada kuangalia mienendo ya miamba au kuta katika maeneo ya uchimbaji.

Pia alimweleza kuwapo chumba maalum cha uokozi chini ya ardhi katika migodi ili kufanya uokozi kunapotokea dharura.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Afya na Usalama Mahali pa Kazi (OSHA), Hadija Mwenda alisisitiza wataendelea kusimamia majukumu yao ipasavyo kwa mustakabali wa maendeleo ya taifa.

“Tutaendelea kuwezesha maeneo ya kazi yawe salama. Suala la usalama na afya ni suala la kujenga tabia na ujengaji tabia ni jambo linatokana na kuelimishwa,” alisema.